Mwamuzi Daniel Nii Ayi Laryea wa Ghana ameteuliwa na Shirikisho la soka barani Africa CAF kuchezesha mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi kati ya Yanga itakayokuwa ugenini kucheza na U.S.M Alger.
Mbali na Laryea CAF pia imewateua Abel Baba wa Nigeria na David Laryea wa Ghana pia kuwa waamuzi wasaidizi katika pambano hilo litakalopigwa Julai 5 huko Algeria.
Pamoja na Yanga na USM Alger, timu nyingine katika Kundi D ni Rayon Sport ya Rwanda na Gor Mahia ya Kenya ambazo pia zitacheza siku hiyo kwenye mchezo ambao utapigwa Kigali huko Rwanda.
Baada ya mechi ya kwanza ugenini Jumapili, Yanga itamenyana na Rayon Sport mjini Dar es Salaam Mei 16 na itakamilisha mechi za mzunguko wa kwanza kwa kuwafuata Gor Mahia mjini Nairobi Julai 18.
Yanga SC inatarajiwa kuondoka nchini kesho kwenda nchini Algeria kwenye jiji la Algiers, tayari kwa mchezo huo wa kwanza wa Kundi D Kombe la Shirikisho la Soka Afrika.