Hatma ya Lulu kubaki uraiani au Gerezani Kujulikana Leo
Wadau wa sanaa ya filamu nchini masikio yao leo yatakuwa katika Mahakama Kuu ambako kutakuwa na tukio kubwa katika tasnia hiyo wakati itakapotolewa hukumu ya kesi inayomkabili mwigizaji maarufu nchini, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu.
Lulu anakabiliwa na kesi ya kumuua mpenzi wake Steven Kanumba bila kukusudia, kinyume cha kifungu cha 195 cha kanuni za adhabu (PC), Aprili 7, 2012, Sinza Vatican jijini Dar es Salaam kufuatia ugomvi wa kimapenzi ulioibuka baina yao.
Hapana shaka kuwa hii ni hukumu ambayo inasubiriwa kwa hamu na wadau wa sheria, sanaa ya uigizaji, wapenzi wa filamu, ndugu, jamaa na marafiki wa mshtakiwa huyo na wa marehemu Kanumba na hata jamii kwa jumla.
Hii inatokana na ukweli kwamba ni moja ya kesi zilizovuta hisia za makundi yote katika jamii tangu kutokea kwa tukio hilo, kushtakiwa kwa msanii huyo, jinsi jamii ilivyokuwa ikifuatilia mwenendo wa kesi pamoja na kuibua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya jamii na hata vijiweni.
Wakati upande wa mashtaka ukidai kuwa Lulu alimuua Kanumba bila kukusudia, Lulu mwenyewe mara zote amekuwa akikana mashtaka hayo akidai kuwa hahusiki kwa vyovyote na kifo cha mpenzi wake huyo.
Hata hivyo, mvutano huo baina ya mshtakiwa huyo na upande wa mashtaka unatarajiwa kuhitimishwa leo na Jaji Sam Rumanyika aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo.
Kama ilivyo ada kwa kesi yoyote, kila upande yaani upande wa mashtaka na wa utetezi (mshtakiwa) utakuwa unatarajiwa moja kati ya mambo mawili; mshakiwa kutiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu au kuachiwa huru.
Hivyo ndivyo inavyotarajiwa kutokea pia kwa hukumu ya msanii huyo itakaposomwa na Jaji Rumanyika na kama mshtakiwa atatiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo au atabaki uraiani kuendelea na maisha kama kawaida, iwapo mahakama haitamtia hatiani.
Kwa vyovyote itakavyokuwa matokeo ya hukumu hiyo yatakuwa na uzito wa pekee kwa msanii huyo kwani ndiyo itakayotoa mustakabali wa maisha yake.
Hii ina maana kwamba iwapo apatikana na hatia, basi atakabiliwa na adhabu, jambo ambalo litabadili historia na mustakabali wa maisha yake kwa jumla, ingawa inategemeana na adhabu atakayopewa.
Lakini iwapo atashinda kesi hiyo, basi yeye ndiye atakayekuwa na furaha kubwa kwa kuwa atakuwa ameepuka adhabu, na hivyo kuendelea na maisha akiwa huru.
Kwa hiyo, wakati wa hukumu hiyo Jaji Rumanyika anatarajiwa ama kumtia hatiani na kumhukumu adhabu au kumwachia huru.
Katika kufanya hivyo, jaji huyo atazingatia ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na mashahidi wa pande zote, yaani upande wa mashtaka na upande wa utetezi pamoja na vielelezo mbalimbali.
Mbali na ushahidi huo na vielelezo vyake, pia Jaji Rumanyika atazingatia sheria zinazoongoza kesi za namna hiyo pamoja na uamuzi wa kesi mbalimbali zilizowahi kuamuliwa zenye mashtaka na hata mazingira yanayofafana nayo.
Katika kesi hasa za mauaji ama ya kukusudia au ya bila kukusudia huwa kuna ushahidi wa aina mbili. Mosi ni ushahidi wa moja kwa moja, yaani ushahidi wa kushuhudia tukio.
Pili, ni ushahidi wa kimazingira. Huu ni ushahidi ambao hakuna shahidi aliyeshuhudia moja kwa moja tukio likitokea, bali mshtakiwa huhusishwa na tukio kulingana na mazingira yaliyokuwapo kabla au wakati wa tukio husika.
Katika kesi ya Lulu, kwa mujibu wa Jaji Rumanyika, upande wa mashtaka umeegemea kwenye aina hii ya pili ya ushahidi wa mazingira, kwani kati ya mashahidi wanne wa upande huo hakuna hata mmoja aliyeshuhudia tukio hilo.
Ushahidi wa upande wa mashtaka unasema Kanumba alifariki dunia kutokana na tatizo la mtikisiko wa ubongo lijulikanalo kwa kitaalamu kama brain concussion, lililosababisha mfumo wa upumuaji kushindwa kufanya kazi baada ya kujibamiza ukutani upande wa kisogoni.
Hivyo upande wa mashtaka unadai kuwa mshtakiwa ndiye aliyesababisha Kanumba kujibamiza ukutani (ukimaanisha kuwa alimsukuma) na hivyo kupata tatizo lililosababisha kifo chake.
Hata hivyo, hakuna shahidi hata mmoja aliyeieleza mahakama kuwa alishudia mshtakiwa akifanya jambo ambalo lilisababisha kifo cha Kanumba, badala yake kuna ushahidi wa kusikia sauti za ugomvi baina ya Lulu na Kanumba chumbani mwa Kanumba.