CCM yamtolea nje Wema Sepetu.....Yasema Haina Taarifa ya Yeye Kurudi
Baada ya Muigizaji Wema Sepetu kutangaza kurudi ndani ya Chama Cha Mapinduzi baada ya kukihama Februari mwaka huu, Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole amesema kuwa chama hicho hakina taarifa yoyote ya kurudi kwa Wema Sepetu.
Polepole amesema CCM ina utaratibu wa mwanachama kujiunga na chama hicho na kuongeza kwamba chama chao siyo daladala kwamba mtu anaweza kupanda na kushuka wakati wowote apendao, na kwamba CCM ina misingi, imani na masharti ya uanachama.
"Kupitia utaratibu na muundo wetu wa chama kwenye shina kisha ataandikwa kwenye orodha ya wanachama kwenye tawi ambalo yeye ni mkaazi," amesema Polepole.
Ameongeza kwamba habari za Muigizaji huyo kurudi ndani ya CCM yeye amepata taarifa mitandaoni kama jinsi watu wengine walivyozipata.
Pamoja na hayo polepole amefafanua kuwa "Ni heri abaki huko huko (Chadema) au akaanzie kule ambako alichukulia kadi yetu, Kuijenga CCM mpya yenye kuheshimu nidhamu ya chama siyo kazi ndogo na inataka viongozi wenye unyenyekevu, watumishi na wanachama wavumilivu. CCM mpya itakuwa chungu kwa baadhi yetu lakini tamu kwa wengi wetu"