Magari ya polisi yaliyokuwa yamekwama bandarini yachukuliwa
Hatimaye magari 50 ya Jeshi la Polisi yalikuwa yamekwama Bandari ya Dar es Salaam tangu mwaka 2015 yamechukuliwa wiki iliyopita.
Novemba 26 mwaka huu, Rais John Magufuli alitembelea Bandari ya Dar es Salaam na kukuta magari ya polisi yakiwa yamekaa bandarini kwa muda mrefu wakati yalitakiwa kukaa hapo kwa siku 21.
Rais Magufuli alimwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi, (IGP) Simon Sirro kuyachukua ili yakafanye kazi iliyokusudiwa.
Leo Jumanne, Msemaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Janeth Ruzagi amesema magari hayo yameshachukuliwa na polisi.
Alisema mamlaka hiyo na polisi wamefikia makubaliano na kuyachukua magari hayo na sasa yameshaondolewa bandarini.
Akizungumzia magari ya polisi, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa amesema ni kweli wameyachukua magari hayo.
Amesema walitii agizo la Rais na kufanya mazungumzo na bandari na sasa wameshayachukua kwa ajili ya kazi mbalimbali za polisi.