Yanga Yasaini Kiungo Hatari wa Kimataifa
WAKATI zikiwa zimebaki siku nne pekee kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa Desemba 15, Kocha wa Yanga, George Lwandamina leo Jumatatu anatarajia kupokea jina la mshambuliaji raia wa DR Congo kutoka kwa mwenyekiti wa usajili wa timu hiyo, Hussein Nyika, ambaye alikuwa nje kwa ajili ya kusaka mshambuliaji.
Nyika alitembelea nchi za Ghana, Congo na Burundi kwa ajili ya kusaka mshambuliaji wa kimataifa ambaye atajiunga na timu hiyo kwa ajili ya kuongeza nguvu kutokana na washambuliaji wa kutumainiwa Amissi Tambwe na Donald Ngoma kuwa majeruhi jambo ambalo limesababisha wawategemee Ibrahim Ajibu na Mzambia, Obrey Chirwa pekee.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga kimesema kuwa Nyika anatarajiwa kukutana na Lwandamina kwa ajili ya kumpa ripoti juu ya aina gani ya mshambuliaji ambaye anaweza kujiunga na timu hiyo baada ya kufanya uchunguzi kwenye nchi za Congo, Ghana na Burundi ambapo alienda kwa lengo la kusaka mshambuliaji.
“Leo Jumatatu, mwenyekiti wetu wa usajili, Hussein Nyika anatarajia kufanya kikao na kocha, Lwandamina kwa ajili ya kumpa mrejesho wa kile ambacho amekutana nacho baada ya kwenda nje kusaka mshambuliaji ambaye kocha anamuhitaji kabla ya dirisha kufungwa.
“Hadi sasa kuna majina ya washambuliaji watatu kutoka nchi za DR Congo, Ghana na Burundi ambapo alienda wiki chache zilizopita kwa ajili ya kuangalia ni nani ambaye anaweza kuwa msaada katika kipindi hiki ambacho fowadi yetu imepungua makali kutokana na baadhi yao kuwa majeruhi,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, alipotafutwa Nyika ili aweze kuzungumzia hilo, hakuweza kupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuita tu bila ya kupokelewa.