WEKUNDU wa Msimbazi Simba wamewasili salama mjini Iringa na mzuka tele wakitokea Morogoro walikoanza safari mchana wa leo wakiwa na kikosi cha wachezaji 24 kwa ajili ya mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya Lipuli FC.
Simba waliweka Kambi ya siku moja Mjini Morogoro kwa ajili ya maandalizi ya mtanange huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini kufuatia matokeo ya sare waliyoyapata Lipuli katika mchezo wa awali dhidi ya Wekundu hao jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na BOIPLUS Meneja wa Wekundu hao Richard Robert wakiwa njiani alisema wachezaji wote wapo tayari kwa mpambano huo na wanajua wanaenda kucheza na timu ngumu ya Lipuli.
“Kila mmoja katika timu anajua tunaenda kucheza na Lipuli, timu nzuri yenye makocha wazuri wanaoifahamu vema Simba lakini morali ipo juu na kwamba hakuna namna zaidi ya kuhitaji pointi tatu ili turudi Dar es salaam tukiwa vizuri kisaikolojia kujiandaa na mechi yetu dhidi ya Yanga.” ali sema Robert.
Wekundu hao wanaongoza msimamo wa ligi kuu wakiwa wamejikusanyia pointi 58 baada ya kushuka dimbani mara 24 huku mahasimu wao wakubwa Yanga wakiwa katika nafasi ya pili na pointi zao 47 ndani ya michezo 22.
