Mbunge wa Mbeya kupitia CHADEMA Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu, amesema alishangazwa na kitendo cha kusikia imepigwa simu kutoka juu, na kueleza kwamba ni lazima yeye na Masonga wavae sare za jela
Akizungumzia suala hilo Sugu amesema kwamba kitendo hicho kilimshangaza kwani kulikuwa kuna watu wengine wengi walikuwa hawana sare na wamefungwa mule muda mrefu lakini walikosa sare, hivyo kitendo cha kulazimishwa yeye ambaye yuko kwa muda mfupi kilikuwa kinamshangaza.
“ Nisiite kujisikia vibaya niite kushangaa, ni siku ambayo maagizo kutoka juu, ilipigwa simu kwamba lazima Sugu avae uniform na Masonga, unaweza ukaona kwamba zaidi ya wafungwa 600 hawana uniform, Sugu yuko pale mmemfunga kwa miezi mitano, anatakiwa kutumikia kama miezi mitatu, lakini unamlazimisha avae uniform, lakini kuna wafungwa pale wamefungwa maisha mamia kwa mamia hawana uniform, kwa nini usiangalie namna ya kuwapatia wale uniform unahangaika na mtu ambaye anapita tu!?”, amesema Sugu.
Sugu ameendelea kwa kusema kwamba kitendo cha yeye kulazimishwa kuvaa sare hakikumkwaza kwani aliona inamsaidia kuhifadhi nguo zake.
“Zilitafutwa siku hiyo hiyo uniform, wakaja wakatuletea uniform ambazo zimevaliwa tukagoma, tukakataa kwa sababu hatuwezi kuvaa nguo ambazo hatujui zimevaliwa na nani, wakaenda kuhangaika kila kona sijui walitoa Segerea, lakini walitumia nguvu kuhakikisha wanatuvalisha uniform, wao walidhani wakimvalisha Sugu uniform ataathirika kisaikolojia, lakini we umeshanifunga kuvaa nguo ni kitu gani, kwanza utanisaidia kutunza nguo zangu", amesema Sugu.
Sugu aliachiwa huru mapema wiki iliyopita kwa msamaha wa Rais baada ya kutumikia kwa muda mfupi kifungo chake cha miezi mitano katika gereza la Ruanda mkoani Mbeya, akiwa na mwenzake Emmanuel Masonga