Kijana mmoja mkazi wa Mbezi Dar es Salaam, Frank Japhet (23) ambaye alijisalimisha katika Kituo cha Polisi Mlandizi, mkoani Pwani, baada ya mzigo wa mahindi unaokadiriwa kuwa na uzito wa kilo 20 aliodaiwa kuuiba kung'ang'ania kichwani, amesimulia mwanzo mwisho kilichomkuta huku akiwaasa vijana wengine wafanye kazi na waache tabia hizo.
Kwa maelezo ya mtuhumiwa huyo aliyoyatoa kituoni hapo, mzigo huo wa mahindi, uliofungwa kwenye kiroba aliuiba kwa mama mmoja eneo la Mtaa wa Nyambwiro, Mlandizi, Kibaha majira ya saa 7.00 usiku wa kuamkia leo.
Amesema, alipoondoka na mzigo huo hadi eneo la stendi ya Mlandizi alipotaka kuacha kwa mwenzake ili arudie mzigo mwingine, ndipo mzigo huo ulipomng'ang'ania kichwani.
Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani Jonathan Shana ameelezea kilichomkuta kijana huyo hadi kufikia hatua ya kuondolewa mzigo huo kichwani na mama anayedaiwa kuhusika.
Kamanda Shana amesema walimuita mama huyo kituoni hapo, na alipofik alifungua zipu ya kijana huyo na kuzungumza maneno ambayo wao hawakuyaelewa, ndipo kijana huyo alipoweza kuushusha mzigo huo.