MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema amesema kitendo cha Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe na viongozi na wabunge wengine wa chama hicho kutakiwa kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kila Ijumaa ni sawa na kwamba wamehukumiwa kifungo cha nje.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipozungumza katika mahojiano maalum na Nipashe kwenye Viwanja vya Bunge hapa Dodoma.
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
Lema ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alisema wabunge na viongozi hao wa Chadema kulazimika kusafiri kwenda Dar es Salaam kila Alhamisi, ili Ijumaa waripoti kwenye kituo hicho cha polisi anaona hakina tofauti kubwa na mtu aliyehukumiwa kutumikia kifungo cha nje.
Mbali na suala hilo, katika mahojiano hayo, Lema pia alizungumzia misukosuko aliyoipitia ikiwa ni pamoja na kuwekwa mahabusu kwa zaidi ya miezi mitatu na mambo mengine ya kitaifa na kifamilia.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano ya Nipashe na mbunge huyo ambaye huu ni muhula wake wa pili bungeni:-
Swali: Kila jambo linapotokea huacha funzo kwa liliyempata na jamii inayomzunguka. Kufungwa kwa Mheshimiwa Sugu kumekupa funzo gani?
Lema: Funzo nililolipata ni kwamba unaweza kupata kesi na kufungwa. Kuna kesi nyingine za kutengenezewa. Na si Sugu pekee yake.
Mimi nimekwenda jela, nimekuta kuna watu wana miaka zaidi ya nane wako mahabusu, kesi zao hazijawahi kukamilika. Tanzania si tu unaweza kufungwa, bali unaweza kukaa hata mahabusu muda mrefu bila sababu za msingi.
Kifungo anachotumikia Sugu ni kifupi kuliko ambacho mimi nimekaa jela kupigania dhamana. Kwa hiyo, unaweza kufungwa na ukanyimwa dhamana.
Mbowe na wenzake ni kama wamefungwa. Kila Ijumaa wanatakiwa kuripoti 'Police Central' Dar es Salaam. Sasa, hebu niambie, Mbunge wa Tarime, Mbunge wa Iringa anatakiwa aripoti Dar es Salaam kila Ijumaa, hicho tayari ni kifungo cha nje.
Kwa hiyo, kila Alhamisi wanaanza kujiandaa kwa safari kwenda kuripoti Dar es Salaam. Mimi hiki nakiona ni kifungo cha nje cha kila Alhamisi na Ijumaa.
Swali: Umekaa mahabusu gerezani kwa muda mrefu. Misukosuko hii imekupa funzo gani?
Lema: Kwanza, imeniongeza imani ya kumwamini Yesu kwa sababu naye alipita katika misukosuko kama hii. Na misukosuko haijawahi kumuua mtu, bali humjenga.
Misukosuko niliyopata imenijenga, imenifanya kuwa mwenye busara, imenifanya kuwa mvumilivu, imenifanya kuujua wajibu wangu vizuri zaidi kuliko wakati mwingine wowote.
Swali: Kwa kukaa mahabusu muda mrefu, kuna athari zipi kwako binafsi na familia yako?
Lema: Inaathiri, baba anapokuwa hayupo nyumbani watoto wanakuwa na 'stress' (msongo wa mawazo), mama anakuwa na stress, wazazi (wako) wanakuwa na stress.
Nafahamu sasa mama yake Sugu (Joseh Mbilinyi, Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), ni mgonjwa wa presha kwa sababu ya mtoto wake.
Watoto tunaweza kuvumilia lakini si kwa wazazi. Watoto pia wanajisikia vibaya, mke anajisikia vibaya, familia, ndugu wanajisikia vibaya, lakini ni suala la muda tu.
Wasipojisikia vibaya sasa, watoto na wajukuu wetu watakuja kujisikia vibaya siku zote na milele ikiwezekana.
Swali: Matumaini ni makubwa kiasi gani kwamba Lema atarejea tena bungeni 2020?
Lema: CCM hawawezi kushinda si Arusha peke yake. CCM hawawezi kushinda uchaguzi Tanzania. Tunahitaji tume huru ya uchaguzi tu. CCM haiwezi kushinda uchaguzi mahali popote.
Arusha...! Sijawahi kuwaza uchaguzi wa mwaka 2020, mimi nawaza vizazi vya taifa hili. Sasa wanaojipanga wala sijawahi kuwafikiria, wala sijawahi kuwatafakari.
Hakuna mtu anayeweza kunishinda Arusha. Na si kwa sababu nina nguvu sana, lakini ni kwa sababu 'commitment' yangu kwa wananchi imekuwa ni ya kiwango cha juu.
Wanaona jinsi ninavyopata shida, napata shida kwa ajili ya nchi, napata shida kwa ajili yao. CCM hawawezi kunishinda Arusha kama ambavyo hawawezi kushinda popote katika nchi hii kwa sasa.
Swali: Ukipata nafasi ya kuzungumza na Waziri Mkuu leo kwa dakika moja, utampa ushauri upi kwa serikali?
Lema: Jambo kubwa ambalo serikali ningependa kuishauri kwa sasa ni kumpenda jirani yako kama unavyoipenda nafsi yako. Ushauri wangu ni huo tu.
Kwamba taifa linaongozwa na upendo, tupendane. Upendo ukikaa kwa dhati katika mioyo ya viongozi wetu na wananchi kwa ujumla, nchi itashamiri.
Haki huinua taifa. Ukisoma maandiko matakatifu, Mfalme Selemani amesema haki huinua taifa. Uchumi wa nchi haujengwi kwa dhahabu, haujengwi kwa makaa ya mawe, nchi inajengwa kwa haki.
Ndio maana kuna mataifa kama Uswisi, hawana madini lakini ni taifa lenye utajiri mkubwa mara milioni moja ya Tanzania.
Mmiliki wa Facebook na mmiliki wa Microsoft ukichukua mitaji yao pengine ni bajeti ya nchi hii kwa miaka 20, lakini hao jamaa hawana dhahabu wala makaa ya mawe, wanajivunia akili zao tu. Tusipopendana tunaumizana.
Swali: Ni miaka mitatu sasa bado kuna mgogoro ndani ya uongozi wa CUF. Una ushauri gani kwa viongozi wa chama hicho ukizingatia ni sehemu ya Ukawa?
Lema: Binafsi sioni tatizo kubwa ndani ya CUF, bali changamoto tu ya baadhi yao kutumika vibaya kwa mkakati fulani wenye lengo la kukiharibu chama hicho na Ukawa.
Lakini naamini mwisho wa siku Maalim Seif atashinda kwa sababu ana wafuasi wengi wanaomwamini Zanzibar na ameanza mapambano muda mrefu, amepambana sana, amekwenda hadi jela muda mrefu kupigania mageuzi. Nafikiri siku moja ipo atafanikiwa.
Swali: Kuna hoja ilitolewa na Joseph Selasini wiki iliyopita kwamba Jeshi la Polisi limepoteza heshima yake. Wewe ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, una kauli ipi juu ya hoja hii?
Lema: Ni ukweli, ni kweli kabisa Jeshi la Polisi limepoteza heshima yake. Mimi ni shuhuda wa Jeshi la Polisi kupoteza heshima yake, ni shuhuda kabisa limepoteza heshima na linapaswa kuundwa upya.
Ni lazima Jeshi la Polisi lisukwe upya, lakini anayelisuka ni nani? Jeshi la Polisi limepoteza heshima kwa sababu linatumika.
Jeshi la Polisi lina 'regulations' zake na lina misingi yake ya kimaadili, lakini sasa inakiukwa kwa sababu linatumika. Wanaolitumia Jeshi la Polisi ndiyo wanaotakiwa wabadilike, hasa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Swali: Kumekuwa na hamahama ya vyama na kujiuzulu kwa viongozi wa upinzani na wengi wanaojiuzulu nafasi zao zikiwamo za ubunge wanatangaza kujiunga na CCM. Tutarajie kuona Lema pia anavua gwanda?
Lema: CCM hawawezi kunifuata mimi na kujaribu kunishawishi kujiunga nao. Wanajua msimamo wangu. Jambo la mwisho na la kwanza ambalo siwezi kulifanya ni kujiunga na CCM.
Siwezi kwenda CCM kwa kushawishiwa kwa cheo wala kitu chochote. Nitaendelea kuwa upinzani na nafurahia kuikosoa serikali kuliko kuwa shabiki wa serikali.