MTIFUANO umetokea kati ya Ofisi ya Bunge na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuhusu siku ya kuzikwa kwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma, Kasuku Bilago.
Marehemu Bilago alifariki dunia Jumamosi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), baada ya kuugua kwa muda mfupi na anatarijiwa kuzikwa katika Kijiji cha Kasuga, Wilayani Kakonko.
Jana, Chadema kupitia kwa Mwenyekiti wake Taifa, Freeman Mbowe ilitangaza keshokutwa kuwa siku atakayozikwa mbunge huyo.
Lakini Bunge juzi lilitangaza kesho kuwa siku ya mazishi baada ya kikao kizito kilichoongozwa na Spika Job Ndugai ambacho ilielezwa kuwa kilikuwa na uwakilishi wa chama hicho.
Aidha, siku ya kesho ilisisitizwa jana na Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai alipozungumza na Nipashe kwa njia ya simu baada ya mabadiliko ya ratiba yaliyotangazwa na Mbowe.
Kagaigai alisema anachofahamu Kamati ya Uongozi ya Bunge ilipitisha kesho kuwa siku ya mazishi.
"Tarehe ambayo mimi Katibu naijua ni Mei 30, mwaka huu na itakuwa ni siku ya Jumatano sasa hiyo unayosema mimi sifahamu... ninachojua ni hicho ambacho kimepitishwa na Bunge," alisema Kagaigai ambaye alisisitiza hajapata taarifa za kubadilishwa kwa siku hiyo.
"Kikubwa ninachoweza kusema tusubiri hiyo siku si bado haijafika? Ndo tutajua marehemu anazikwa siku gani lakini ninachofahamu ni Jumatano."
Mwili wa marehemu Bilago utapelekwa bungeni leo kwa ajili ya wabunge kutoa heshima zao za mwisho.
Jana wakati wa misa ya kuaga mwili wa marehemu Bilago katika Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam, Mbowe alisema marehemu atazikwa keshokutwa na si kesho kama Ofisi ya Bunge "inavyotaka".
"Juzi tulifanya kikao na familia ya marehemu, tukaafiki azikwe siku ya Alhamisi, tumewapa Bunge taarifa hiyo lakini bado wanalazimisha tumzike Jumatano," alisema Mbowe na kuweka msimamo:
"Wasitulazimishe. Kama hawataki tutashughulikia mazishi peke yetu.
"Kama tuliweza kumtibia (Tundu) Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki) kwa nini tushindwe kumzika Bilago?"Hiyo siku ya Jumatano wanayoitaka watamzika mtu wao lakini Bilago atazikwa Alhamisi."
Mbowe alisema Bunge linaundwa na sehemu mbili ambazo ni Serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi na Kambi Rasmi ya Upinzani inayojumuisha vyama vya CUF, ACT-Wazalendo, Chadema na NCCR-Mageuzi.
Alisema katika mahusiano ya kibinadamu wabunge wa vyama vya upinzani bungeni wanaishi kwa kuelewana lakini upande wa pili urafiki wao umekuwa wa mashaka.
"Bilago alifariki mchana, jioni siku hiyo hiyo Ofisi ya Bunge ikatangaza ratiba ya mazishi bila ya kushirikiana na familia wala chama chake," alisema.
"Wakati huo hatujakaa kikao, hatujawasiliana na ndugu na familia, bila ya 'consultation' (mashauriano) Ofisi ya Bunge inatoa ratiba ya mazishi, jambo hilo limetukwaza sana.
"Wangekuwa wanampenda marehemu Bilago wangemtibia."
MARA MWISHO
Mbowe alisema mara ya mwisho kuwasiliana na marehemu Bilago Jumatano iliyopita akiwa safarini kuelekea Afrika Kusini.
Alisema marehemu alimtumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS) uliokuwa ukimuomba kufika kumuona Muhimbili, kuona tatizo la ugonjwa wake pamoja na kumshauri.
"Marehemu Bilago alikuwa anahitaji msaada wa haraka kwenda kutibiwa nje ya nchi, nilirudi nchini Ijumaa, nikaenda Muhimbili Jumamosi nikakuta hali yake ni mbaya," alisema zaidi mwenyekiti huyo.
"Wakati tukifanya utaratibu wa kumsafirisha, mchana siku ya Jumamosi akakata kauli, madaktari walijitahidi kwa takribani nusu saa kuokoa maisha yake lakini hawakufanikiwa."
Akisoma wasifu wa marehemu, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji alisema marehemu Bilago alikuwa anaugua ugonjwa wa mshipa.
Alisema marehemu alizaliwa Februari 2, 1964 katika kijiji cha Kamhasha wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.
Alisema alisoma elimu ya msingi katika shule mbalimbali kuanzia mwaka 1975-1982, alisoma Shule ya Sekondari Kigoma mwaka 1983-1986 na alisomea stashahada ya ualimu Monduli Arusha mwaka 1987-1990
Pia, alisomea Shahada ya Falsafa chuo cha Newcastle nchini Uingereza mwaka 2005-2006, pamoja na Shahada ya uzamili ya mahusiano ya kimataifa Uingereza mwaka 2006-2007.
Dk. Mashinji alisema marehemu Bilago alipata mafunzo ya kitaaluma ya uongozi mwaka 1990-1996, aliwahi kuwa Katibu wa Chama Cha Walimu (CWT) mkoa wa Mbeya 1996-2005, Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema na Mwenyekiti wa Kanda ya Magharibi, Mbunge wa Jimbo la Buyungu 2015 mpaka mauti yalipomkuta.
Akiongoza ibada ya kuombea mwili wa marehemu Bilago, Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Magomeni, Christian Nyumayo alisema marehemu Bilago siku aliyofariki ndiyo alitarajia kufanya maadhimisho ya miaka 25 ya ndoa yake.
Aidha, aliwataka Watanzania kuishi kwa kumkumbuka Mungu, kufuata utaratibu pamoja na kufahamu kuwa tupo safarini.
MAMBO MENGI
Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Yeremia Maganja alisema marehemu Bilago alitengeneza mambo mengi katika uhai wake, ikiwamo kutokutaka tamaa kwa viogozi wa vyama.
Mwakilishi wa CWT, Mathew Komba alisema marehemu akiwa Katibu wa CWT Mbeya alihamasisha umoja na undugu katika jumuiya hiyo.
Mtumishi ofisi ya Bunge, Mbariki Masinga alisema marehemu Bilago alikuwa ni mnyenyekevu wakati wote akiwa bungeni.