HAKUNA kitu kizuri duniani kama kujielewa kuwa umekosea na kurekebisha makosa. Pia katika maisha hakuna binadamu aliyekamilika pale linapokuja suala la kukosea.
Inaeleweka kuwa, kwa muda mrefu wazazi wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, mzee Abdul Jumaa ‘Baba Diamond’ na Sanura Kassim ‘Bi Sandra’ walikuwa na tofauti za muda mrefu na hivi karibuni tofauti zao zinajionesha wazi kuisha licha ya kila mmoja kuwa katika uhusiano mwingine.
DIAMOND NA MZEE ABDUL
Mzee Abdul aliingia kwenye bifu zito na Diamond baada ya kumtuhumu kutomjali kwa sababu tu ana ugomvi na mama yake mzazi, (Bi Sandra) hali iliyosababisha staa huyo anayebamba na Ngoma ya African Beauty kumchunia kwa muda mrefu.
Hayo yote yalijidhihirisha wazi pindi tu Diamond alipofanikiwa kupata mtoto wake wa kwanza, Latiffah Nasibu ‘Tiffah’ aliyezaa na mjasiriamali, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ siku aliyokuwa anamtoa nje kwa mara ya kwanza ‘Arobaini’ ambapo Diamond hakumwalika mzee Abdul hali iliyofanya baba huyo kuhuzunika.
Siyo Tiffah tu, bali hata mpenzi wake huyo wa zamani, Zari alipojifungua mtoto wao wa pili, Nillan pia hakupelekwa kwa babu yake.
MOBETTO ASAFISHA NJIA
Baada ya hali hiyo kuendelea, mwanamitindo Hamisa Mobetto naye alipojifungua mtoto wa kiume, Dylan Nasibu aliyezaa na Diamond aliamua kusafisha njia kwa kumualika mzee Abdul kwenye hafla ya kumtoa nje mtoto wao kwa siku ya kwanza ili mwanaye aweze kupata baraka za babu yake pia.
BI SANDRA ‘ASANDA’
Baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu huku kila mmoja akikwepa kumzungumzia mwenzake kwa vyovyote, juzikati Bi Sandra alionesha ‘kusanda’ kwa kuamua kumuanika mzee Abdul mitandaoni.
Kupitia ukurasa wa Instagram wa Bi Sandra, aliweka picha ya muda mrefu ya mzee Abdul akiwa amembeba Diamond alipokuwa mdogo, kitendo kilichofanya komenti kibao kujazana katika ukurasa huo.
“Nasibu kichwa na mzee Abdul…namuona Nillan Mtupu,” aliandika Bi Sandra.
DIAMOND AINGILIA KATI
Muda mfupi baada ya picha hiyo kupostiwa, Diamond aliingia katika komenti ya picha hiyo na kuweka hisia zake kwa kuandika; “Dah! Hii picha nilikuwa ninaitafuta sana…kuna picha moja nimembeba Nillan kama hivyo nilitaka nizimix halafu niwawekee maboya wanaokazania kusema Nillan siyo mwanangu…”
MZEE ABDUL AFUNGUKA
Baada ya sarakasi hizo zote, Ijumaa Wikienda lilimtafuta mzee Abdul ili kuzungumzia ishu hiyo ambapo alisema yeye hana tatizo lolote na watoto wake ambao ni Nasibu na Mwajuma Abdul ‘Queen Darleen’.
“Kama mama Diamond kafanya hivyo, basi ujue mimi ni mzazi mwenzake, Diamond tumemlea, tumeishi naye kwa muda mrefu na hayo masuala mengine yaliotokea kipindi cha katikati ni ya kifamilia tu na naimani ni mapito,” alisema mzee Abdul.
AGUSIA MALI
“Pia shida za kifamilia zipo tu, hazina matatizo yoyote, kama masuala ya mali ni yake, lakini kama ananitambua mimi baba yake, basi ni baba yake, ina maana kama hizo mali ni zake siwezi nikamuingilia, ipo siku akitaka kunipa atanipa asipotaka basi, huwezi ukamfosi,”alimaliza mzee Abdul.
WALIPOTOKA
Tatizo la Diamond kutoelewana na mzee Abdul limekuwa likitikisa kwa muda mrefu huku kila mmoja akimtupia lawama mwenzake, hivyo kitendo cha mama Diamond kumposti mzazi mwenzake huyo ina maana ya kuwa sasa wako sawa na hawana tofauti zozote zinazoendelea kati yao.