ZAINAB IDDY NA MARTIN MAZUGWA
KIPA wa Simba, Said Mohamed ‘Nduda’, yupo njiapanda kuendelea kuitumikia klabu hiyo kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano mengine.
Nduda alisajiliwa na Simba msimu uliopita akitokea Mtibwa Sugar, lakini alishindwa kuidakia kutokana na kuandamwa na majeraha kwa kipindi kirefu.
Taarifa ambazo BINGWA limezipata kutoka ndani ya Simba, zinasema kuwa kutokana na kipa huyo kushindwa kuisaidia timu hiyo wapo mbioni kuachana naye.
“Wapo wachezaji wengi ambao Simba hatutaendelea nao msimu ujao akiwamo Nduda na hii imetokana na mchango wake kuwa mdogo katika timu,” kilisema chanzo chetu.
BINGWA lilimtafuta Ndunda kujua kama anataarifa za kutemwa, alisema hadi sasa hana anachojua kuwa ana mkataba wa mwaka mmoja zaidi.
“Sijui lolote juu ya jambo hilo, lakini siwezi kukataa iwapo wakiamua kuvunja mkataba wangu uliobaki kwa kigezo cha kutoisaidia timu, hili ni kweli na sababu inajulikana wazi nilikuwa majeruhi.
Kama tutaendelea kufanya kazi pamoja sawa na wakiamua kuvunja sawa, kuwapo ndani ya kikosi cha Simba msimu ujao yapo kwa benchi la ufundi na viongozi,” alisema.