HOUSE OF ENTERTAINMENT


JOIN KENYASWAHILINEWS
!-- AdsAgony - Ad Display Code -->

MPYA MPYA ZA LEO

HABARI (193) Michezo (121) BURUDANI (86)

Jumamosi, 19 Mei 2018

Shahidi adai Nondo aliwasiliana na Mange Kimambi


Iringa. Kesi inayomkabili mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abdul Nondo iliendelea jana, huku shahidi wa upande wa Jamhuri akidai kuwa Februari 25 mshtakiwa huyo aliwasiliana kwa barua pepe na Mange Kimambi.

Nondo ambaye pia ni mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSN), alikamatwa Machi 8 akidaiwa kudanganya kuwa alitekwa na watu wasiojulikana.

Akitoa ushahidi mbele ya hakimu mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, John Mpitanjia, ofisa upelelezi wa makosa ya mitandao ambaye pia ni shahidi namba tano, koplo Abdulkadir alisema aligundua kuwa Nondo aliwasiliana na Mtanzania huyo aishiye Marekani.

Aliieleza mahakama hiyo kuwa aligundua mawasiliano hayo baada ya kuifanyia uchunguzi simu ya mshtakiwa ambapo alikuta ujumbe wa barua pepe kwenda kwa Mange ukimwambia kuwa yeye ni Nondo, mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania.

Shahidi huyo alidai ujumbe huo pia ulisema yeye ndiye aliyezungumza na baadhi ya vyombo vya habari kuhusiana na kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.

“Ujumbe huo pia ulisema, amepata tetesi kuwa anatafutwa na watu wasiojulikana na kushauriwa asitembee peke yake kwa sababu ana hatihati ya kutekwa,” alidai koplo Abdulkadir.

Pia aliieleza mahakama hiyo kuwa Nondo alituma ujumbe saa 9:09 mchana siku ya tukio kwa kutumia simu ya mkononi kupitia mtandao wa Whatsap kwenda ka Paul Kisabo akiwa Ubungo uliosomeka “am at risk” .

Kadhalika, shahidi huyo alidai alikuta namba tatu za simu ambazo hazikupokewa katika simu ya Nondo ambazo zilipigwa kati ya saa nane mchana hadi 3:45 usiku.

Kwa upande wake, shahidi namba mbili koplo John alisema alimpokea mshtakiwa huyo katika Kituo cha Polisi Mafinga na kuandikisha maelezo yake.

Shahidi huyo alisema baada ya kuchukua maelezo hayo alibaini kuwa Nondo hakutekwa kama upelelezi wa koplo Abdulkadri ulivyobaini na hivyo waliamua kuripoti suala hilo katika uongozi wa juu.

Baada ya mashahidi hao wawili kutoa ushahidi, hakimu Mpitanjia aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 12 na 13.

Source: mwananchi