TIMU ya Simba ya jijini Dar es Salaam imesema kuwa inahitaji kucheza soka la ushindani na la kiwango cha juu katika mechi zote nne zilizobakia katika Ligi Kuu Tanzania Bara licha ya kuhitaji pointi tano tu ili kutangazwa mabingwa wapya wa msimu wa mwaka 2017/18.
Simba ambayo inadhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa imebakiza mechi dhidi ya Ndanda FC, Singida United, Kagera Sugar na itafunga dimba ugenini Songea kwa kuwavaa wenyeji Majimaji Mei 28 mwaka huu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, alisema kuwa timu yake haiwazi kusaka pointi tano, inachofikiria ni kuhakikisha inashinda mechi zote zilizobakia za ligi hiyo inayotoa mwakilishi wa Tanzania Bara katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kocha huyo raia wa Burundi alisema kuwa mbali na "kiu" ya kutwaa ubingwa waliyonayo, pia wanataka kuona wanavunja rekodi ya kutofungwa kama ambavyo iliwahi kuwekwa na Kocha Mzambia, Patrick Phiri kwenye kikosi hicho.
"Tumebakisha mechi chache lakini zina changamoto sana, tunataka kuona kasi tuliyoanza nayo wakati ligi inaanza ndiyo tunamaliza nayo, ingawa si jambo rahisi kwa sababu kila timu sasa inajua inahitaji pointi ili kujiweka mahali salama, " alisema Djuma.
Mbali na Simba, timu nyingine ambazo ziko katika vita ya kuwania ubingwa wa Bara endapo zitashinda mechi zake zote zilizosalia ni mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC na mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga, zote za Dar es Salaam.
Katika mechi nne zilizobakia za vinara hao, mbili watacheza nyumbani dhidi ya Ndanda FC itakayofanyika kesho kwenye Uwanja wa Taifa na nyingine itawakaribisha Kagera Sugar huku ikisafiri kwenda Singida na Ruvuma.
Endapo Simba itatwaa ubingwa huo, inamaana kuwa mwakani Yanga haitashiriki michuano yoyote ya kimataifa baada ya watani hao wa jadi kutolewa mapema kwenye mashindano ya Kombe la FA ambayo yanatoa tiketi ya kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.