HOUSE OF ENTERTAINMENT


JOIN KENYASWAHILINEWS
!-- AdsAgony - Ad Display Code -->

MPYA MPYA ZA LEO

HABARI (193) Michezo (121) BURUDANI (86)

Jumamosi, 9 Juni 2018

Mbowe na Zitto wasusiwa



VYAMA  vya siasa vitano vyenye wabunge na visivyo na wabunge, vimewaingiza mtegoni  Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na aliyekuwa hasimu wake kisiasa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),  Freeman Mbowe. RAI linaripoti.


Viongozi wa vyama hivyo  vitano, kila mmoja kwa wakati wake alionesha kukubaliana na uamuzi wa Mbowe na Zitto wa kuanzisha Muungano wa kisiasa wenye lengo la kusimamisha mgombea mmoja kwenye chaguzi zijazo, wakianzia na jimbo la Buyungu, lakini baadhi yao waliwataka waanzisha wazo hilo kujitathimini na kupima imani zao kabla ya kushirikisha wengine.


Aidha, ili kufanikisha nia hiyo walipendekeza kuitishwa kwa kikao cha pamoja ili kulijadili suala hilo kwa kina kabla ya kuanza kufanyiwa kazi, lengo likiwa ni kukwepa usaliti.


Viongozi wa NCCR-Mageuzi,  CUF, TLP, NLD na Chauma kila mmoja ametoa kauli zilizobeba mitego ya namna yake kwa  Zitto na Mbowe.


MREMA- TLP


Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labor Party (TLP), Agustine Mrema alisema yupo tayari kushiriki katika umoja huo mpya, lakini ni lazima ushirikiano huo uwe shirikishi na jumuishi kwenye kila hatua.


“Hakuna mtu anayekataa ushirikiano, lakini kama wanataka kushirikisha vyama vingine ni lazima wajipime na pia tuupime ukweli wao, je, huo muungano ni sustainable (endelevu), na ni inclusive (shirikishi), hatutaki umoja wa kinafki!.


“Nia yao ni nzuri, kwani umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu, lakini hizo hatua wanazozichukua, zinatakiwa kuwa za dhati zinazotoka kwenye mioyo yao kwa sababu tumewahi kushuhudia muungano kama huu  ukifa na kuua vyama vingine, unakuta watu wanadanganyana kuungana, lakini hawana ukweli mioyoni mwao, mwisho unaishia katika kununua wajumbe wa upande mwingine,  au wanafika nusu njia wanaanza malumbano,” alisema


Pamoja na hilo, Mrema aliendelea kumlaumu James Mbatia kwa kudai kuwa aliteuliwa na Ukawa, lakini hana alichokifanya, badala yake analalamikiwa na wananchi katika jimbo hilo licha ya awali kuwa na matumaini naye.


Alipoulizwa kama bado ana ndoto za kuwania jimbo hilo, Mrema alisema kwa sasa hayuko tayari kutupa silaha zake hadharani.


NCCR -MAGEUZI


Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi, Juju Danda aliliambia RAI kuwa wao wanaamini umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, hivyo umoja mpya wa Chadema na ACT- Wazalendo si mbaya na haupaswi kuwa chanzo cha kuvuruga vyama vingine.


Alisema wao hawawezi kukizuia Chadema mshirika wao kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kushirikiana na ACT- Wazalendo  kusimamisha mgombea katika jimbo la Buyungu, lakini tahadhari inatakiwa.


Alisema kimsingi makubaliano ya Ukawa hayazuii chama chochote kuungana na chama kingine, hivyo ni haki ya Chadema kuungana na ACT-Wazalendo.


“Chama kinaweza kushirikiana na mwingine ili mradi asiathiri mambo ya msingi ambayo tumejiwekea ni sawa na nchi mwanachama wa SADC anaweza kushirikiana na EAC ila lazima mambo ya msingi yaweze kusimamiwa vema,” alisema.


Alisema kama Chadema imeona kuna umuhimu wa kutanua ushirikiano kwa kuangalia jimbo hilosi wazo baya, lakini wao  NCCR wanaangalia zaidi ushirikiano wa nchi nzima.


“Hoja ya msingi ni kwamba anayehitaji kujiunga na Ukawa ni lazima atume ombi la kutaka kuwa mshirika na wale wanachama wamjadili, umoja huu hauamuliwi na chama kimoja, haya ni mambo ambayo tunaamua kuanzia kwenye vikao vyetu,” alisema.


CUF-PROF. LIPUMBA


Mwenyekiti wa CUF, anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba alisema kwa kuwa hajapewa taarifa rasmi kuhusu umuhimu wa muungano huo, hawezi kubainisha kuwa yupo tayari kuungana nao au lah!


“Sijapewa taarifa yoyote kwa hiyo sijui taratibu zake zipoje, kwa sasa siwezi kusema lolote kwa kuwa sijapewa taarifa rasmi na viongozi ambao wanaanzisha umoja huo,” alisema.


Hata hivyo Prof. Lipumba alisema kwa kuwa wahusika ni viongozi wa vyama vya upinzani na wametangaza hatua hiyo hadharani, ni vema wakafanya mazungumzo ya kina na wenzao juu ya mpango na sababu za  muungano huo ili viongozi wa vyama vingine vya upinzani waweze kutoka na kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu misimamo yao.


Aidha alisema chama chao kwa sasa kinaombeleza kifo cha mbunge Bilago hivyo hawafikirii namna ya kupambana, badala yake watafikiria kusimamisha ama kutosimamisha mgombea baada ya Tume ya Uchaguzi (NEC) kutangaza tatarehe ya uchaguzi mdogo katika jimbo hilo.


Wakati Prof. Lipumba akisema hivyo tayari Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Mji Mkongwe (CUF), Ismail Jussa ameunga mkono muungano huo na kusema kuwa lengo linapaswa kuwa pana zaidi ya kuunganisha vyama.


Jusa ambaye anaunga mkono CUF – Maalim Seif, alisema; “Umoja anaouzungumzia Zitto unahusisha pia makundi mbalimbali zaidi ya vyama vya siasa. Kwa mfano kuna wakulima, wafanyakazi na mimi naongezea waandishi wa habari, asasi za kiraia, makundi ya kidini na watu wote wenye nia njema,” alisema.


MASHINJI NA UKAWA


Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, alisema katiba ya chama chao  inaruhusu chama kuungana na wadau wowote ambao wanafanya mambo yanayofanana bila kujali mdau huyo anatokea wapi, lakini kwa sasa tumaini lao ni Ukawa.


“Ukawa ndio tumaini letu, ndio maana tuko hatua za awali za mazungumzo na hao wengine, ila lengo ni kuwaambia wananchi wetu tumejipanga kupambana na hawa maadui. Kikubwa sisi kama watendaji tunaanda utaratibu ili kuona muungano huo ufanyike vipi,” alisema.


Kuhusu hofu ya usaliti, alisema taarifa za usaliti na kukosekana kwa uaminifu kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa ni jambo linalohitaji uchunguzi wa kina.


“Mtu kuwa active kuhamasisha muungano ni jambo la kheri sana kwa sababu wote adui yetu ni mmoja ambaye ni CCM. Katika uanzishwaji wa kitu chochote kuna wazo, halafu unalijaribu, ukishalijaribu unalitengenezea mpango mzima, kwa hiyo tupo kwenye hatua za awali sana.


KATIBU MKUU NLD


Katibu Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD), TozziMatwanga aliunga mkono kauli ya umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, ila ametoa wito kwa viongozi hao wa Chadema na ACT-Wazalendo, kuitisha kikao cha uasisi wa pamoja ili kuangalia masilahi mapana ya vyama vyote.


“Tutaangalia misingi ya umoja huo kwani NLD siku zote ni wamoja ndio maana tukasimama na wenzetu ndani ya Ukawa, ila kwa kuwa hatujahakikishiwa nadhani Mbowe na chama chake wataandaa taarifa.


‘Suala la kusema tunaunga mkono ama lah halijawa wazi kiasi hicho cha kusema tunaunga mkono ghafla tu.  Lazima kuangalia taratibu za muungano ambao unakuwa kwa masilahi ya vyama vyote si vilivyoasisi.


“NLD siku zote tumekuwa wamoja, tumesikia wenzetu wameungana na Zitto hatujajua nafasi ya Mbowe au Zitto au kama ni rasmi ila sisi tunaona hakuna ubaya,” alisema.


KATIBU MKUU  CHAUMA


Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma),  Eugine Kabendera alisema umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, hivyo dhamira yao ni kuona upinzani unashika dola, lakini ni lazima umakini uwepo.


“Kuna namna nyingi ya kushika dola, ingawa tunaweza kushika wenyewe kama chama kimoja, lakini Chauma tunaamini sana katika umoja hivyo kama watatushirikisha nadhani hatuna pingamizi tutashirikiana, lakini ni vema ikawepo mijadala ili kuona tunaelekea wapi kwani ni jambo lenye kheri,” alisema.


Mwaka jana Chauma kiliungana na Chadema kususia chaguzi ndogo katika majimbo mbalimbali nchini na wameahidi kuendelea kuungana na vyama vingine vya siasa kwenye mnambo ya msingi.


Wachambuzi wa masuala ya siasa wanaziona tahadhari hizo za viongozi wa vyama vingine ni mtego kwa Mbowe na Zitto ambao vyama vyao havijawahi kushirikiana katika harakati za kisiasa kabla na hata baada ya kuanzishwa kwa Ukawa.


Hofu inayotawala uimara wa UDF ni historia za waasisi wake kuonekana kutokuwa na ushirikiano wa dhati kisiasa hasa baada ya kutofautiana walipokuwa ndani ya Chadema.


Aidha kuteketea kimya kimya kwa Ukawa, umoja uliokuwa na nguvu kubwa ya ushawishi kwenye Bunge Maalum la Katiba na hata wakati wa uchaguzi Mkuu mwaka 2015 nako kunatajwa kuwa eneo jingine linalotia shaka uendelevu wa UDF.


UJIO WA UDF


Wazo la muungano huo linatajwa kuibuliwa na Zitto, ambaye kwa kushirikiana na Mbowe walilitangaza rasmi mkoani Kigoma wakati wa shughuli za mazishi za aliyekuwa Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago (Chadema) aliyefariki Dunia Mei 26, mwaka huu.


Viongozi wa vyama hivyo viwili wakizungumza na waombolezaji katika uwanja wa Mbwenge walitangaza kuungana na kumsimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Buyungu- wilayani Kakonko mkoani Kigoma katika hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).


Mbowe alisema kifo cha Bilago lazima kiwaunganishe wakazi wa Kakonko na Watanzania kwa ujumla hivyo aliwataka  wananchi wamuunge mkono yeye na Zitto.


Baada ya kusema hayo alimuinuaZitto – Mbunge wa Kigoma mjini, ambaye alikubali kushirikiana na Chadema kusimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi huo


Awali katika mitandao ya kijamii Zitto alisema amekuwa na dhamira ya kuona vyama hivyo vikiunganisha nguvu dhidi ya CCM katika chaguzi mbalimbali, hivyo yeye na Mbowe wamekubaliana kushawishi kuwapo kwa ushirikiano wa vyama vya upinzani katika uchaguzi huo mdogo.


“Kwa heshima ya Mwalimu Bilago mimi na Mbowe tumekubaliana kuwa tutawashawishi kuwapo na United Democratic Front (ushirikiano wa kidemokrasia) katika jimbo la Buyungu. Huo ni mwanzo wa harakati za kuwa na ushirikiano wa kidemorasia dhidi ya ukandamizaji wa demokrasia nchini hali mbaya ya maisha ya wananchi,” alisema Zitto.


Aidha, siku moja baadaye Mbowe alifafanua kuwa umoja huo hautakuwa wa utani kwa sababu hautanganisha vyama vilivyosajiliwa zaidi ya miaka 20 lakini havina hata mwenyekiti wa serikali ya mtaa.


“Chadema siku zote tunasema tuko tayari kushirikiana na chama chochote ikiwa ni pamoja na kugawana majimbo kama tulivyofanya Ukawa, lakini tunashirikiana na vyama vyenye thamani, kwa mfano CUF tunashirikiana na upande wa Maalim seif na vingine vitakavyoonesha nia hiyo,” alisema Mbowe.


Hata hivyo kauli hiyo ya Mbowe ilimsukuma Zitto kutoa tahadhari na kumtaka mshirika wake huyo mpya kisiasa, kutobagua vyama vingine badala yake waimarishe nguvu ili kulinda demokrasia ya vyama vingi nchini na kwamba jambo la muhimu ni kuweka vigezo na washirika wavifuate bila ubaguzi.


UDF AFRIKA


Umoja wa namna hiyo hautakuwa wa kwanza barani Afrika, kwani mwaka 1983 wakati wa harakati za kupambana na ubaguzi wa rangi, makundi mbalimbali yaliyohusisha makanisa, wanafunzi, wafanyakazi na taasisi nyingine nchini Afrika Kusini waliungana na kupambana na makaburu.


Aidha mwaka 1992, aliyekuwa Rais wa Malawi, Bakili Muluzi alianzisha chama cha siasa kilichojulikana kama UDF.