Maajabu: Tajiri Aliyeshinda Mnada Nyumba za Lugumi kwa Blioni 3.3 Anaishi Nyumba ya Kupanga....Kodi Kwa Mwezi ni 50,000
Imebainika kuwa Dk. Shika anakaa kwenye nyumba hiyo iliyopo Mtaa wa Amani kwa kipindi cha takribani mwaka mmoja sasa na kodi anayolipa kwa mwezi ni takribani Sh. 50,000.
Aidha, baadhi ya majirani zake wamemuelezea kuwa ni mtu asiye na makeke, huku baadhi wakidai kuwa aliwahi kuwaahidi wauza mihogo ya kukaanga walio jirani na mahala anapoishi kuwa atawaunganishia kupata mikopo nafuu ili wakuze biashara zao, lakini bila ya kuwatajia taasisi atakayowaunganisha nao. Inadaiwa kuwa vilevile, kwa baadhi ya watu hufahamika kwa jina la ‘profesa’.
Dk. Shika alijipatia umaarufu katikati ya wiki baada ya kuibuka mshindi katika mnada wa nyumba za kifahari za Lugumi, kwa kununua nyumba moja ya Mbweni kwa Sh. bilioni 1.2, nyumba ya pili iliyoko pia Mbweni Sh. milioni 900 na nyumba ya tatu iliyoko Upanga alishinda na kutaka kununua kwa Sh. bilioni 1.2.
Hata hivyo, alishindwa kutumiza masharti ya kulipa asilimia 25 ya fedha kwa kila nyumba baada ya kushinda, hivyo kujikuta akitiwa mikononi mwa vyombo vya dola kwa kuharibu mnada.
Katikati ya wiki hii, jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, lilimtia nguvuni Dk. Shika kutokana na tuhuma za kuharibu mnada huku likidai kuwa linafanya uchunguzi zaidi ili kubaini kwa nini alifanya hivyo.
Mbali na kuchunguza juu ya hatua ya kuharibu mnada, kamanda wa kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema walikwenda nyumbani kwake kufanya upekuzi sambamba na kuchunguza udaktari wake. Shika aliwahi kukaririwa kuwa ni msomi wa shahada ya uzamivu (Ph.D).
Hata hivyo, Mambosasa alisema udaktari wake huo unatia shaka kwa kuwa ameshindwa kuonyesha vielelezo kuthibitisha kama anastahili hadhi hiyo.