HOUSE OF ENTERTAINMENT


JOIN KENYASWAHILINEWS
!-- AdsAgony - Ad Display Code -->

MPYA MPYA ZA LEO

HABARI (193) Michezo (121) BURUDANI (86)

Ijumaa, 10 Novemba 2017

Selasini ataka mbunge wa CCM Achunguzwe Sakata la Tundu Lissu Kupigwa Risasi

Selasini ataka mbunge wa CCM Achunguzwe Sakata la Tundu Lissu Kupigwa Risasi


Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini ameomba Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga ahusishwe katika uchunguzi wa tukio la kushambuliwa Tundu Lissu.

Selasini ametoa ombi hilo bungeni mjini Dodoma jana  Alhamisi Novemba 9,2017 jioni akichangia mjadala wa mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/19 na mwongozo wa maandalizi ya mpango na bajeti kwa mwaka 2018/19.

Mbunge huyo wa Rombo akichangia alisema mbunge huyo alishahusishwa na mauaji ya mpenzi wa mpenzi wake, hivyo ni vyema akahusika na uchunguzi huo.

Baada ya mbunge huyo kueleza hayo, Mlinga aliomba kwa Spika ampe taarifa Selasini akisema katika kipindi cha uhai wake hajawahi kuhusishwa na mauaji.

“Ninamheshimu sana mheshimiwa Selasini. Tangu nizaliwe sijawahi kuhusishwa na kifo cha mpenzi wa rafiki yangu namuomba alete ushahidi katika Bunge hili ni nani alinihusisha,” alisema Mlinga.

Mwenyekiti wa Bunge, Nagma Giga alimuuliza Selasini kama anapokea taarifa hiyo lakini mbunge huyo aliendelea kushikilia msimamo wake akisema suala hilo liliandikwa katika gazeti la Dira.

“Nimemsikia na huo ni mkuki kwa nguruwe lakini kwa binadamu ni mchungu. Gazeti la Dira liliandika vizuri sana kuwa mpenzi wako alikusaliti. Wewe na kundi la vijana wenzako mkaenda kumuua. Liliripotiwa polisi na limeripotiwa kwenye magazeti na hujawahi kukanusha hadi leo,” alisema.

Selasini alisema, “Ningeiomba Serikali katika uchunguzi wa nani waliohusika kutaka kudhulumu maisha ya Tundu Lissu, huyu ambaye ameshatajwa kwamba alihusishwa na mauaji uchunguzi uanzie kwake,” alisema.

Mbunge huyo wa Rombo alisema asubuhi wakati Mlinga alipoomba mwongozo wa Spika, mwongozo wake ulijaa kejeli na kumhusisha Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na mauaji ya albino.

Katika mwongozo huo, Mlinga alihoji hatua ya Mbowe kutaka wachunguzi wa kimataifa kuchunguza tukio la Lissu aliyejeruhiwa kwa risasi Septemba 7 mjini Dodoma na kuhoji ni kwa nini hakuwahi kutaka wachunguzi hao katika mauaji ya albino.

Mlinga alisema kwa kuwa kuna taarifa kuwa wapo wanasiasa wanahusika na mauaji ya albino basi Mbowe naye ni mhusika na pia akasema ni kwa nini hakuhoji mauaji ya watu wa Kibiti na Rufiji.

Hata hivyo, Spika Job Ndugai alisema kwake haoni kama kuna mwongozo na kuelekeza shughuli za Bunge ziendelee kwa wachangiaji kuanza kuchangia mpango huo.

Asubuhi katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, Mbowe alimuomba waziri mkuu akubali wachunguzi wa kimataifa waje nchini kuchunguza tukio la kushambuliwa Lissu ambaye anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema bado vyombo vya kiuchunguzi nchini havijashindwa kuchunguza tukio hilo na akawahakikishia Watanzania kuwa uchunguzi unaendelea.