Klabu ya soka ya AFC Leopards ya nchini Kenya imetuma ofa kwenda klabu ya Dar Young Africans ya jijini Dar es Salaam ikihitaji huduma ya mlinzi wa pembeni Mwinyi Haji Mngwali.
Mngwali ambaye ametia fora akiwa na timu ya soka ya Taifa ya Zanzibar katika michuano ya soka ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’ kwa kuonesha kiwango bora anawania na miamba hiyo ya soka ya Kenya pamoja na wachezaji kadhaa wa Zanzibar heros.
Akiitumikia Zanzibar Heroes Mngwali ameisaidia timu hiyo kufika hatua ya fainali kwa kucheza michezo yote ya makundi ambapo mchezo pekee ambao Mngwali aliukosa ulikuwa mchezo wa nusu Fanali dhidi ya Uganda ambapo Zanzibar ilishinda kwa mabao 2-1.
Aidha mbali na AFC Leopards pia klabu ya soka ya Gor Mahia wameonekana kuvutiwa na kiungo Abdulazizi Makame Hassan ambaye naye alikuwepo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Zanzibar kinachoshiriki michuano ya CECAFA.
Taarifa zinasema kuwa Gor Mahia walimfuatilia mchezaji huyo toka Zanzibar walipocheza na Tanzania Bara, na tayari benchi la Ufundi la miamba hiyo ya soka ya Kenya wamempendekeza kuwapo katika kikosi chao.
Aidha Makame alifunga bao la kwanza katika mchezo wa nusu fainali ya michuano ya CECAFA, pale Zanzibar walipoichabanga Uganda kwa mabao 2-1 mchezo ambao ulipigwa kwenye uwanja wa Moi mjini Kisumu nchini Kenya.