Wanajeshi waliomng'oa Mugabe madarakani wateuliwa Baraza la Mawaziri Zimbabwe
Rais mpya wa Jamhuri ya Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa ametangaza baraza la mawaziri ambapo amewateua viongozi wakuu wa jeshi la nchi hiyo katika nafasi mbalimbali.
Katika baraza hilo lililotangazwa Novemba 30, Mnangagwa amemteua Meja Jenerali Sibusiso Moyo kuwa Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi.
Moyo ndiye alitangaza katika kituo cha runinga cha Taifa (ZBC) kuwa jeshi limechukua udhibiti wa nchi wakati Rais Mugabe alipowekwa kizuizini nyumbani kwake.
Aidha, Mkuu wa Jeshi la Anga la Zimbabwe, Perence Shiri ameteuliwa katika baraza hilo na kuwa Waziri wa Kilimo na Masuala ya Ardhi. Mnangagwa aliapishwa juma lililopita kuwa Rais wa Zimbabwe baada ya Robert Mugabe kukubali kujiuzulu.
Wakati akihutubia mjini Harare baada ya kuapishwa, Mnangagwa aliahidi mabadiliko makubwa, lakini baraza lake la mawaziri limekosolewa vikali kutokana na uwepo wa viongozi hao wa jeshi.
Jeshi la Zimbabwe limekuwa na mchango mkubwa katika aina ya siasa za nchi hiyo, na mara kadhaa limekuwa likikosolewa kwamba, lilimsaidia Rais Mugabe kukaa madarakani kwa miaka 37.
Mbali na uteuzi wa wanajeshi hao, lakini pia baraza hilo limekosolewa kwa kuwapo kwa baadhi ya watu ambao walikuwa na uhusiano na Rais Mugabe, mfano Chris Mutsvangwa ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari.
Wengi waliotoa maoni yao wamesema kuwa hatua hiyo imewakatisha tamaa kwa waliamini uwepo wa kiongozi mpya ungeifanya nchi hiyo kupata viongozi wapya ambao wangesaidia kuitoa Zimbabwe hapo ilipo sasa.