Klabu ya Singida United imetinga fainali ya kombe la FA (ASFC) baada ya kuilaza JKT Tanzania kwa mabao 2-1 kwenye mchezo uliopigwa katika uwanja wa Namfua mkoani SIngida.
Kiungo Tafadzwa Kutinyu alifunga mabao yote ya Singida United wakati bao la JKT Tanzania lilifungwa na Hassani Matelema.
JKT Tanzania ndio ilianza kufunga bao la kuongoza kwenye dakika ya 38 kabla Kutinyu hajaifungia Singida United kwenye dakika za 54 na 98.
Mchezo huo ulichezwa kwa dakika 120.
Kulikuwa na mkanganyiko wa kanuni ambazo hata hivyo inaelezwa kuwa zimefanyiwa mabadiliko kwa michuano ya mwaka huu.
Wachezaji wa JKT Tanzania walikuwa wameanza kujipanga tayari kwa mikwaju ya penati kabla hawajaelezwa kuwa mchezo huo utaendelea kwa dakika 30 za nyongeza
Singida United sasa itachuana na Mtibwa Sugar Juni 02, 2018 katika mchezo wa fainali utakaopigwa kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha.
Mshindi wa mchezo huo atajinyakulia kitita cha Tsh Mil 50 pamoja na kuwa muwakilishi wa Tanzania Bara kwenye michuano ya kombe la Shirikisho Barani Afrika.