TANZANIA ni nchi pekee katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inayotumia mitambo ya kisasa ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia (combined cycle).
Mitambo hiyo ina uwezo wa kuchoma gesi hiyo na kuzalisha umeme pamoja na kutumia mvuke wake, kuzalisha megawati nyingine. Nchi ina mitambo sita ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia, miwili ikiwa na mitambo hiyo ya kisasa ya kutumia mvuke pia kuzalisha umeme, ambayo inasaidia kuzalisha umeme zaidi kuliko mitambo ya kawaida.
Meneja miradi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Stephen Manga alisema mitambo hiyo ya kisasa iliyozinduliwa hivi karibuni na Rais John Magufuli katika mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi II, ina uwezo wa kuzalisha Megawati 240.
Alisema katika mitambo hiyo, megawati 167.82 inazalishwa baada ya kuchomwa gesi asilia na megawati nyingine 80.4 zinazalishwa baada ya hewa ya joto nyenye nyuzi 550 kuchanganywa na maji kidogo na kutoa mvuke kisha kuzalisha umeme.
“Katika mitambo ya zamani umeme huo wa mvuke unaachwa na kupotea, lakini sasa tumezana kuzalisha na umeme huo siyo mdogo, kwani una uwezo wa kuhudumia mikoa miwili ya Arusha na Kilimanjaro na wilaya zake zote,” alisema. Manga alisema hiyo ndiyo tofauti baina ya mitambo hiyo, kwani kunakuwa na umeme wa ziada unaozalishwa na kwa sasa ni wa kwanza nchini na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Alieleza kuwa pia mitambo mingine itakayotumia gesi asilia ya Kinyerezi III utakaozalisha megawati 600 na Kinyerezi IV megawati 330, inaofuatia utekelezaji wake utakuwa wa aina hiyo, huku wakifikiria na mingine ya Somanga wilayani Kilwa, Lindi na kwingineko na hivyo kuachana na mitambo ya kuzalisha umeme ya kawaida isiyotumia mvuke pia.
Akizungumzia mpango wa serikali kuuza umeme katika nchi za Afrika Mashariki, katika mradi wa msongo wa kilovoti 400 kwa umbali wa kilometa 414, alisema tayari wakandarasi wanaendelea na utekelezaji wa mradi wa kuunganisha umeme kutoka Singida, Manyara mpaka nchini Kenya.
“Mradi huu wa kuuza umeme katika nchi za Afrika Mashariki unaendelea vema na wakandarasi wameshapatikana na baada ya kufika nchini Kenya tutapeleka mpaka Uganda na baadaye nchi nyingine zote za EAC na umeme huu utajumuisha unaozalisha kwa teknolojia mbalimbali,” alisema.
Katika kupeleka umeme nje ya nchi, siyo EAC pekee bali pia kuna mradi wa kutoka Iringa, Mbeya na Tunduma mkoani Songwe mpaka Zambia, ambao nao uko katika hatua nzuri. Ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi II ulizinduliwa Machi, 2016 na kujengwa na kampuni ya Sumitomo Corporation ya Japan.
Umekamilika siku 45 kabla ya muda uliopangwa, kutokana na serikali kutoa Sh bilioni 120 na mkopo wa gharama nafuu kutoka Japan wa dola za Marekani milioni 292.4 na kufanya mradi huo kugharimu dola za Marekani milioni 344 sawa na Sh bilioni 758. Alisema miradi mingine iliyo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ni Mtwara megawati 300 na ule wa maporomoko ya maji ya Bonde la Mto Rufiji maarufu kama Stiegler’s Gorge wa megawati 2,100.
Mbali na miradi hiyo, kuna mradi wa upanuzi wa Kinyerezi I utakaozalisha megawati 325 kutoka megawati 150 za sasa, unaoendelea kwa gharama ya Sh bilioni 400 na utakamilika mwanzoni mwa mwaka ujao. Inaelezwa kuwa mwaka 2004 utaendelea kubaki katika kumbukumbu za nchi katika sekta ya nishati, ambapo kwa mara ya kwanza Tanzania ilianza kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia.
Miaka 14 baadae, Tanzania imeendelea kuwa kinara katika nchi za Afrika Mashariki, ambazo zinatumia gesi asilia kuzalisha umeme ambapo hadi sasa zaidi ya asilimia 50 ya umeme unaozalishwa nchini unatokana na nishati ya gesi asilia.
Mitambo ya kufua umeme ya Kinyerezi II, ina uwezo wa kuzalisha megawati 240 za umeme na inategemea gesi asilia inayozalishwa na kusambazwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kupitia kampuni tanzu ya Gasco, inayosimamia shughuli za ukusanyaji na usambazaji wa gesi asilia nchini.
Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alieleza mipango ya wizara yake katika kufikia Tanzania ya viwanda kwa kutumia gesi asilia kuzalisha umeme wa uhakika.
“Ufunguzi wa Kinyerezi II ni muendelezo wa miradi ya umeme wa gesi asilia, baada ya mradi wa leo tunategemea kutekeleza miradi mingine miwili hapa Kinyerezi ambayo yote itatumia gesi asilia na kuzalisha megawati 600, isitoshe tunatarajia kuzalisha umeme wa gesi asilia pale Somangafungu megawati 320 na kule Mtwara megawati 300,” alisema.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Kapuulya Musomba alisema TPDC imejipanga kuhakikisha gesi asilia inaendelea kupatikana kwa wingi ili kuwezesha Tanzania ya viwanda, sio tu kwenye umeme, bali hata kwenye viwanda moja kwa moja ambapo hutumika kama chanzo cha nishati au malighafi.