Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi nchini (TSNP) Abdul Nondo amefunguka na kusema kuwa kigezo cha bodi ya mikopo kutoa mikopo kwa kuzingatia tu wanafunzi waliosoma shule za serikali na kuwabagua wale waliosoma shule za private si sawa kwa kuwa kufanya hivyo ni kuwakosesha haki watu kusoma.
Abdul Nondo amesema hayo siku moja baada ya kauli ya Rais Magufuli kusema kuwa bodi ya mikopo haiwezi kutoa mikopo kwa wanafunzi ambao awali walionekana kusoma katika shule za binafsi na kudai kuwa watu hao wanauwezo hata wa kusomesha na wazazi wao ndiyo maana waliweza kusomeshwa katika shule binafsi walipokuwa wakisoma.
"Mara ya kwanza kabisa, niliwahi sikia kauli ya namna hiyo kwa Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Maimuna Tarishi akisema kama umesoma private school hupati mkopo. Kauli hii tuliipinga vikali, kipindi hicho na tukasema sio fair sababu gharama za chuo ni kubwa (Ada, hela ya kula ,copy, usafiri,hela ya malazi, hela ya mafunzo kwa vitendo field). Ni tofauti kabisa na fedha ya ada shule ya private laki 8, au mil 1 ambayo pia watu husoma kwa ada hiyo private. Kuwanyima mkopo ni kuwakatishia ndoto zao kabisa"
Nondo aliendelea kusema kuwa sababu nyingine ni kuwa uwezo wa mzazi unaweza kubadilika badilika inawezekana kipindi cha nyuma alikuwa na uwezo wa kulipia gharama lakini kipindi mtoto anaingia chuo labda mzazi amepatwa na magonjwa ya kudumu, uchumi umeyumba kiasi cha kushindwa kumudu gharama hizo jambo ambalo linapelekea wanafunzi wengine kukosa haki ya kusoma elimu ya juu.
"Mfano kipindi mtoto akiwa anasoma 'private' mzazi alikuwa na uwezo wa kulipa, kipindi mtoto anaingia chuo baba au mzazi amepata magonjwa, ameparalyze, amefilisika, kumnyima mkopo mtoto huyu ni kumkatishia malengo yake. Pia tulihoji juu ya kama mtoto amesoma kwa kudhaminiwa inakuwaje, kuna wanaodhaminiwa kusoma private schools na mashirika binafsi, watu binafsi, na husomeshwa shule tuu sio chuo, baadaye hutelekezwa chuo wajitegemee. Hii bodi ya mikopo walisema wataweka kipengele kuambatanisha vielelezo vya udhamini ila huwa ni geresha tuu huwa hawatoi hata uambatanishe ndio maana sio sahihi kutoa mkopo kwa kigezo cha u private schools, au u government schools siyo haki"
"Tulihoji pia wapo waliosoma kwa kurUdia mitihani kutafuta 'credits' mara nyingi hawa huwekwa katika kundi la private schools, wapo QT (qualified Tests), wapo diploma wote hawa huwa termed as private schools. Kuwanyima mkopo kwa vigezo hivi ni kupoteza ndoto zao. Kigezo cha kutoa au kutotoa mkopo kwa kuangalia ulisoma private au government sio kigezo sahihi. Kime katisha ndoto za wanafunzi wengi saana sababu hakitoi majibu halisi ya uwezo wa mwanafunzi kustahimili gharama"
Mbali na hilo Abdul Nondo amesema bodi ya mikopo sasa imekuwa ikikusanya marejesho ya mikopo kuliko kipindi chote kama ambavyo wao wenyewe wamekuwa wakisema hilo hivyo amewaomba kigezo hicho cha kuangalia mwanafunzi alisoma shule gani na kumpa mkopo huku wengine wakikosa mkopo kutokana na shule walizowahi kusoma siyo haki na kuwa kitendo hicho ni kukatisha ndoto za watu kusoma elimu ya juu.
"Hakuna kipindi bodi ya mikopo wanakusanya makusanyo na marejesho Kama kipindi hiki, tuwasii bodi ya mikopo hiki kigezo hakifai. Kama bodi ya mikopo wataamua kukitumia kama kigezo cha kukosa mkopo, basi tunawaomba waandike katika muongozo wao wa 2018/2019 .Wakiongeze kuwa "Kama ulisoma shule ya binafsi hupati mkopo" ili wazazi wajipange mapema na wajue kuwa mtoto akisoma private school hapati mkopo kutoka bodi ya mikopo. Itasaidia ikifafanuliwa hivyo"