Kitendo cha beki wa Yanga Kelvin Yondani kumtemea mate mchezaji wa Simba Asante Kwasi katika mchezo wa watani wa jadi Jumapili iliyopita, kinaendea kujadiliwa kwenye mitandao ya kijamii pamoja na vyombo mbalimbali vya habari.
Yondani alifanya tukio hilo bila kuonekana kwa waamuzi wa mchezo huo lakini camera za Azam TV zilinasa mkasa mzima wa tukio hilo.
Wadau mbalimbali wametoa maoni yao kwa nyakati tofauti kuhusu kitendo cha Yondani kumtemea mate Kwasi. Wengi wamelaani na kupinga vikali jambo hilo pamoja na kushauri adhabu itolewe kwa kufuata kanuni na taratibu zilizopo.
Musa Kisoki-Mwenyekiti chama cha wachezaji wa mpira wa miguu Tanzania SPUTANZA
Ni kitendo cha utovu wa nidhamu kwa kiwango alichofikia Kelvin Yondani hautegemei kumuona akifanya vitendo vya kijinga kama vile, wachezaji wetu ifike mahali wajitambue nini mpira unataka, kanuni na taratibu za mpira.
Unapofanya vitendo vya utovu wa nidhamu unajishushia heshima mwenyewe, unapochaguliwa hafi timu ya taifa unatakiwa ujitambue.
Kanuni zipo wazi nadhani ni kanuni ya 37 inaeleza adhabu kwa wachezaji (mchezaji yeyote akifanya kitendo kichume cha maadili na mwenendo wa soka adhabu yake ni kufungiwa mechi tatu na faini ya shilingi laki tano.
Tukiwa tunachelewesha hizi adhabu tunawafanya watu wengine waje kulalamika kama kuna upendeleo. Kitu kimetokea kimeonekana piga adhabu palepale.
Oscar Oscar-Mchambuzi
Tusitengeneze mazungira ya kutetea kitendo cha Yondani kumtemea mate Kwasi kwamba kuna wakati wachezazi wana-panic au wanakuwa na presha ya mchezo. Sio kitendo ambacho kinapaswa kuungwa mkono kwa namna yoyote ile.
Tanzania tumekuwa na double standards kwa baadhi ya vitu, hiki ambacho amekifanya Yondani kwa Asante Kwasi kuna muda huwa nafikiria ingekuwaje kama kingefanywa na Juma Nyoso?
Mimi nilitarajia watu wa kwanza kumkemea na kumuadhibu Yondani ilipaswa kuwa klabu yake kwa sababu wao ndio waajiri wake.
Yanga walipaswa kuwa wa kwanza kumwadhibu Yondani pamoja na kuomba radhi kwa sababu kuomba radhi kutokana na kukosea ni kitendo cha uungwana, wamuombe radhi Kwasi kwani kuna tatizo gani?
Chirwa alikuwa na kesi ya kumpiga mwandishi wa habari mazoezini, ikafichwafichwa matokeo yake tunatengeneza mwendelezo wa hawa watu kuendelea kufanya matukio ya utovu wa nidhamu kwa sababu hawaadhibiwi.
Wasiadhibiwe kwa kuwakomoa, waadhibiwe kwa maana ya funzo ili wengine waone na wajifunze kwamba hata wao wakifanya makosa wataadhibiwa.
Ally Mayay-Mchambuzi
Matukio yoyote ambayo si ya kinidhamu au ya uvunjifu wa sheria yanatakiwa kupingwa kwa nguvu zote, lakini kingine inatakiwa kutolewa elimu kwa wachezaji watambue kwa dunia ya sasa mchezaji hawezi kufanya tukio uwanjani asionekane.
Kila mmoja kwa nafasi yake kwa ajili ya kutoa elimu kwa wachezaji kucheza mpira wa kuzingatia sheria na kusitokee matukio kama haya ambayo yanauchafua mpira wa miguu.
Kanuni zipo ambazo zinatoa adhabu lakini wachezaji wanatakiwa watambue hasa wachezaji wakubwa ambao wana heshima na uzoefu wa kutosha.