Comments Off on Kondakta aliyeokota na kumrudishia abiria sh 600,000 azua gumzo
‘Kondakta’ wa daladala nchini Kenya maarufu kama ‘Matatu’ aliyegeuka gumzo mitaani na kwenye mitandao kwa kitendo cha kurejesha pochi ya abiria aliyoiokota ikiwa na sh 30,000 za Kenya (Sawa na sh 680,000 za Tanzania) amepata neema ya kusomeshwa, kugharamiwa matibabu ya mkewe na mengine.
Kondakta huyo alieleza kuwa aliiokota pochi ya abiria huyo, akaipeleka katika kituo cha polisi na kubaki na fedha ambazo baada ya kumpata mmiliki alimrejeshea huku akikataa kupokea zawadi yoyote ya uokotaji.
Kutokana na hatua hiyo ya uaminifu ambao wengi hawakuutegemea, mwanzilishi wa kipindi maarufu cha ucheshi cha ‘Churchill Show’ alimemuahidi kumempa zawadi ya aina yake ya kumrudisha shule na kumalizia masomo ya TEHAMA baada ya kumueleza jinsi alivyoingia kwenye kazi ya ukondakta baada ya kuacha chuo kwa kukosa karo.
Mwaura ambaye ni baba wa mtoto mmoja anayetarajia kumpata mtoto wa pili kwani mkewe ni mjamzito, alisema kuwa aliamua kuacha chuo mwaka 2011 alipokuwa anachukua masomo ya TEHAMA katika chuo cha Kenya Polytechnic kutokana na kukosa karo na kushindwa kumudu gharama nyingine za masomo.
Mwaura atarudi katika chuo hichohicho na kuendelea na masomo yake ya TEHAMA, lakini sasa chuo hicho kimebadili jina na kinafahamika kama Chuo Kikuu cha Ufundi cha Kenya (Technical University of Kenya).
Mbali na neema hiyo, amekuwa akipokea zawadi za fedha kutoka kwa watu mbalimbali kwa jinsi walivyoguswa na uaminifu wake pamoja na zawadi nyingine ya matibabu ya mkewe na mtoto, pamoja na kuhudumiwa gharama zote za mkewe wakati wa kujifungua na wiki kadhaa za matunzo ya kichanga.
Mkasa wa kukota na kurejesha pochi yenye ‘ukwasi’ ulivyokuwa:
Abiria aliyejulikana kwa jina la Stanley Kaberi alipanda ‘matatu’ Ijumaa ya Aprili 11, lakini kwa bahati mbaya aliangusha pochi (wallet) yake ndani ya gari hilo iliyokuwa na vitambulisho pamoja na sh 30,000 za Kenya.
Siku iliyofuata, alienda kuripoti katika ofisi za polisi kuhusu upotevu wa pochi na vilivyokuwa ndani yake, lakini alipofika aliambiwa kuwa tayari Mwaura alikuwa amefika katika ofisi hiyo kuripoti kuhusu kuokota pochi hiyo na aliwataka wawasiliane naye kama mtu yoyote atajitokeza.
Mwaura alisema kuwa baada ya kupigiwa simu kuwa Stanley amefika akidai kuwa pochi hiyo ni yake, aliwasiliana naye na kukutana katika kituo kimoja. Baada ya kumuona, alitambua kuwa mtu huyo ndiye Stanley aliyemuona kwenye kitambulisho kilichowekwa kwenye pochi aliyoikota, hivyo akajiridhisha kuwa ndiye mmiliki halali.
“Nilimuuliza ni kitu gani kingine ambacho kilikuwa kwenye pochi hiyo, aliponitajia kiwango halisi cha sh 30,000 niliamini ndiye na nikampa pesa hizo ambazo nilikuwa nazo, sikuziacha kituoni nikimsubiri mmiliki halali nimpe,” alisema Mwaura.
Alisema kuwa baada ya kumpa fedha hizo, Stanley alitaka kumpa kiasi fulani kama shukurani yake kwa kumuokoa na shida ya kupoteza fehda, lakini alikataa na kumtaka alipie kwanza bili ya matibabu ya mwanaye ambaye anakabiliwa na matatizo ya kiafya.
Ni uaminifu wa aina yake, kwa kondakta ambaye hakuwa na fedha za kugharamia matibabu ya mkewe anayetarajia kujifungua, lakini hakuwa na tamaa ya shilingi 680,000 kwa ‘chenji’ ya Tanzania. Hakuwaza kuwa pochi hiyo ya ukwasi ilikuwa zawadi kutoka kwa Mungu kumsaidia, bali alifikiria hali ya mmiliki halali wa pochi hiyo.
Kwa kitendo hicho, Mwaura amegeuka kuwa mtu maarufu mwenye sifa ya uaminifu uliotukuka, picha yake na sifa zake zimesambaa mitandaoni na huenda akapata ‘mchongo’ wa kufanya kazi katika moja kati ya makampuni makubwa kama balozi mwaminifu.