Gadiel aliyesajiliwa na Yanga mwanzoni mwa msimu huu akitokea Azam FC, ameliambia gazeti hili kwamba sababu hasa inayomtamanisha kwenda Ufaransa ni urahisi wa kuonwa na timu nyingine kubwa zaidi Ulaya.
BEKI wa kushoto wa Yanga, Gadiel Michael, amefichua mipango yake ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi huku akitaja Ligi ya Ufaransa kama chaguo lake la kwanza.
Gadiel aliyesajiliwa na Yanga mwanzoni mwa msimu huu akitokea Azam FC, ameliambia gazeti hili kwamba sababu hasa inayomtamanisha kwenda Ufaransa ni urahisi wa kuonwa na timu nyingine kubwa zaidi Ulaya.
“Kama ikitokea nafasi hiyo, Ligi ya Ufaransa nadhani ndio sehemu nzuri zaidi kwenda kucheza kwa sababu inavyoonekana timu nyingi zinaangalia kule, lakini pia hata wachezaji wa Ufaransa wanaonyesha wanapigiana chapuo pindi wanapoenda kwingine,” alisema Gadiel.
“Ndoto ya kucheza soka la kulipwa Ulaya bado ipo kwani bado nina umri sahihi na naamini nina kipaji cha kunifikisha huko,” alisisitiza beki huyo anayeichezea Taifa Stars pia.
Tangu alipojiunga na Yanga, beki huyo amejihakikishia nafasi ya kudumu kwenye klabu yake na timu ya taifa ambapo amekuwa kama chaguo la kwanza upande wa beki wa kushoto.
Gadiel aliibuka mwaka 2012 kwenye mashindano ya soka kwa vijana wenye umri wa miaka isiyozidi 17 ya Copa Coca Cola.
Ikumbukwe mashindano ya mwaka huo ndio yaliwaibua pia Aishi Manula, Joseph Kimwaga, Farid Mussa, Mohammed Hussein pamoja na Miraji Adamu.