
WIKIENDI iliyopita, Simba iliendelea kuandika rekodi katika Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kufanikiwa kuifunga Yanga bao 1-0 kwenye mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Ulikuwa ni mchezo ambao uligusa hisia za wengi na kuwa na mambo mengi, lakini dakika 90 ndizo ziliweza kuamua mambo yote kwenye mchezo huo.
Lakini katika mchezo huo baadhi ya wachezaji wa Simba na Yanga waliweza kufanya vema kutokana na kuonyesha viwango bora, huku wengine wakipotezwa.
Baadhi yao licha ya kuwa na majina makubwa lakini walishindwa kuonyesha makali yao kwenye mchezo huo kama ambavyo imezoeleka katika michezo mingine.

Wafuatao ni baadhi ya wale ambao waliweza kuonyesha viwango bora kwenye mchezo huo.
JONAS MKUDE –SIMBA
Alikuwa ndiye mhimili mkuu kama siyo nguzo kwa upande wa Simba na aliweza kupambana na kutoa pasi ambazo zilifika vizuri kwa walengwa.
Mkude alipambana kwa kiasi kikubwa na kufanikiwa kuiendesha timu na kuisaidia kuondoka na pointi zote tatu. Katika nafasi ya kiungo wa kati, alimpiku Papy Tshishimbi wa Yanga.

KELVIN YONDANI – YANGA
Licha ya timu yake kushindwa kupata matokeo mazuri, lakini uwezo wake wa kupambana kwa kiasi kikubwa uliweza kuonekana katika harakati za kuiokoa Yanga isipoteze mchezo.
Licha ya ubora wake ndani ya dakika tisini, Yondani hakufanya uungwana pale alipomtemea mate beki wa Simba, Asante Kwasi.

ERASTO NYONI – SIMBA
Ndiye aliyefanikiwa kuibeba zaidi Simba kutokana na bao lake alilolifunga dakika ya 38 kwa kichwa.
Bao la Nyoni katika mchezo huo limeendelea zaidi kuiweka Simba kwenye nafasi nzuri ya kuwania ubingwa msimu huu.
Nyoni alifunga bao hilo ukiwa ni mchezo wake wa pili wa ‘derby’ hiyo tangu ajiunge na Simba msimu huu akitokea Azam FC.
Katika mchezo huo alionekana kuwa bora kutokana na kiwango ambacho aliweza kukionyesha na uwezo wake wa kucheza nafasi zaidi ya moja anapokuwa uwanjani.
H A S S A N KESSY – YANGA
Licha ya kupewa kadi nyekundu baada ya kumchezea vibaya Asante Kwasi, lakini kwa muda aliocheza wa takriban dakika 48, alikuwa moto kwani aliweza kupambana vyema kwa kusaidia safu ya ulinzi.
Kessy kwa namna fulani aliweza kuwadhibiti Emmanuel Okwi na Shiza Kichuya ili wasilete madhara katika lango lao.

SHIZA KICHUYA – SIMBA
Mechi ya mzunguko wa kwanza ndiye aliyefunga bao kwa Simba katika sare ya 1-1. Safari hii ameshindwa kufunga lakini wikiendi iliyopita licha ya kutofunga, ndiye aliyetengeneza bao lililofungwa na Erasto Nyoni na kuipa ushindi Simba wa bao 1-0.
Mara kadhaa Kichuya amekuwa msumbufu kwa wachezaji wa timu pinzani na ubora wake kila siku umekuwa ukionekana kuwa juu.
YOUTHE ROSTAND – YANGA
Ni kipa wa Yanga na licha ya kufungwa bao katika mchezo huo, lakini tunaweza kumtaja kuwa ni mmoja wa mashujaa wa Yanga kutokana na kazi ya ziada aliyoweza kuifanya ili timu yake isifungwe mabao mengi.
Haikuwa kazi rahisi kuweza kuokoa lakini alipambana na kuweza kuruhusu bao moja pekee na kama Yanga wangekuwa na kipa ambaye si imara basi huenda tungeshuhudia mabao mengi zaidi.
ASANTE KWASI – SIMBA
Sifa yake inajulikana ni beki pekee mwenye mabao mengi mpaka sasa katika Ligi Kuu Bara na kwenye mchezo dhidi ya Yanga aliweza kupambana vyema kwa kuweza kuwathibiti wapinzani wao.
Ulikuwa ni mchezo wake wa kwanza kucheza dhidi ya Yanga akiwa na jezi za Simba, lakini kiwango chake hakikuwa cha kubeza japo alikiona cha moto kutoka kwa beki mwenzake Yondani ambaye alimfanyia kitendo kibaya cha kumtemea mate.
SHOMARY KAPOMBE – SIMBA
Alisaidiana vema na Mkude katika nafasi ya kiungo wa kati. Kapombe na Mkude waliweza kuibeba zaidi Simba kwenye nafasi hiyo ambapo Kapombe aliyezoeleka kucheza beki wa kulia, alifanya kazi ya ziada kuivuruga Yanga.