Mlinda lango chipukizi wa kikosi cha Yanga Ramadhani Kabwili amejiunga na timu ya Taifa ya Vijana Ngorongoro Heroes inayojiandaa na mchezo wa kusaka tiketi ya kufuzu fainali za michuano ya AFCON 2019 kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 dhidi ya Mali.
Mchezo huo utapigwa kwenye uwanja wa Taifa Jumapili, May 13 2018.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia ndiye aliyeagiza kipa huyo kujumuishwa kikosi cha Ngorongoro Heroes baada ya 'kuenguliwa' na kocha Ammy Ninje.
Ninje alimuondoa Kabwili kwenye kikosi chake baada ya kudai uongozi wa Yanga haukufuata taratibu walipomchukua na kusafiri nae nchini Algeria.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo kwenye ukumbi wa mikutano wa TFF, Karia amesema kwamba Kabwili amekwishajiunga na wenzake kambini kuendelea na maandalizi ya mchezo wa Jumapili dhidi ya Mali kufuzu Fainali za Afrika za U20 mwakani nchini Niger.
“Kilichotokea hadi kabwili kwenda nchini Algeria kuitumikia timu yake ya Yanga kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya U.S.M Alger ni kutokuwa na mawasiliano mazuri kati ya uongozi wa TFF na uongozi wa klabu ya Yanga,”amesema.