Dar es Salaam. Wawakilishi hao wa Tanzania, Yanga wameondoka na kikosi cha wachezaji 18, bila ya nahodha wake Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani na Thaban Kamusoko kuelekea Algeria kwa mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi dhidi ya USM Algeria.
Hii ni mara ya kwanza kwa Yanga kusafiriki bila ya manahodha wake hao jambo linaloacha maswali kulikoni ndani ya klabu hiyo kwa sasa.
Yanga ambayo mwishoni mwa wiki ilikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa watani zao Simba imeondoka ikiwa na wachezaji wengi chipukizi katika mchezo huo muhimu.
Yanga yenye rekodi mbaya kila inapocheza mechi za hatua ya makundi mara mbili imemaliza ya mwisho.
Kocha Noel Mwandila na msaidizi wake Shadrack Nsajigwa watabidi kufanya kazi ya ziada kutegeneza kikosi imara kitakachowavaa USM Alger hapo Jumapili.
Wachezaji wa Yanga waliondoka na timu ni Rostand Youthe, Ramadhan Kabwili, Hassan Kessy, Andrew Vincent, Haji Mwinyi, Gadiel Michael, Pato Ngonyani, Said Makapu, Juma Abdul, Yussuf Mhilu, Mwashiuya Geoffrey, Pius Buswita, Rafael Daud, Yohana Nkomola, Emmanuel Martin, Juma Mahadhi, Abdallah Shaibu 'Ninja', na Said Makapu.