Mshambuliaji Quadri Kola Aladeokun kutoka klabu ya Mbabane Highlanders ya Swaziland anatarajiwa kutua leo kufanya majaribio katika klabu ya Yanga imefahamika.
Kola raia wa Nigeria amependekezwa na kiungo wa Yanga Papi Kabamba Tshishimbi aweze kuongezwa kwenye kikosi cha Yanga kinachoshiriki michuano ya kombe la Shirikisho.
Taarifa zaidi zimebainisha kuwa kocha Mwinyi Zahera ndiye aliyeagiza kuletwa kwa mshambuliaji huyo ili aweze kumuona kabla ya kuruhusu asajiliwe.
Kola alikuwa akifuatiliwa na Yanga tangu wakati wa dirisha dogo la usajili mwishoni mwa mwaka jana.
Kama Zahera ataridhishwa na kiwango chake, kusajiliwa kwake huenda ukawa mwisho wa mshambuliaji Donald Ngoma ambaye amekuwa nje kwa zaidi ya miezi saba akisumbuliwa na majeraha ya goti.
Lakini Yanga italazimika kumlipa Ngoma 'mamilioni' ili kuweza kuvunja mkataba wake ambayo unamalizika mwezi Julai mwaka 2019.