Na.mwanaspoti.co.tz
Mkongomani huyo ambaye aliinoa Yanga kwa siku takribani sita kabla ya kuikabili Simba, amesema mambo yatakaa sawa kwani, kupoteza dhidi ya watani wao wa jadi hakuna maana kuwa timu yao imepoteza mwelekeo.
MAMBO hayajakaa sawa na mashabiki wa Yanga ni kama wameanza kuikatia tamaa timu yao. Kiwango kibovu na kupoteza mchezo dhidi ya Simba vimewashtua, lakini kocha wao mpya, Mwinyi Zahera, amewasikia na kuwaomba kutuliza hasira.
Mkongomani huyo ambaye aliinoa Yanga kwa siku takribani sita kabla ya kuikabili Simba, amesema mambo yatakaa sawa kwani, kupoteza dhidi ya watani wao wa jadi hakuna maana kuwa timu yao imepoteza mwelekeo.
Yanga ilipokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Simba juzi Jumapili na kufikisha idadi ya mapambano sita dhidi ya watani zao hao bila kupata ushindi.
Mechi ya mwisho Yanga kushinda dhidi ya Simba ilikuwa Machi 2016 waliposhinda 2-0. Mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara wamekuwa na kiwango cha hovyo, ambapo wamecheza mechi nne dhidi ya Singida United, Welayta Dicha ugenini, Mbeya City na Simba bila kuonja ladha ya ushindi.
Zahera, ambaye alitua nchini wiki iliyopita lakini akashindwa kukaa benchi kwenye mechi dhidi ya Simba kutokana na kutokuwa na vibali vya kazi, alisema amegundua tatizo la msingi la timu hiyo na atalifanyia kazi ndani ya siku saba tu, kisha mambo yatakwenda sawa.
Kocha huyo ambaye kabla ya kujiunga na Yanga alikuwa Kocha Msaidizi wa timu ya Taifa ya DR Congo, alisema Yanga ingeweza kuifunga Simba lakini mapungufu ya kikosi chake hasa wachezaji kutokuwa fiti yaliifanya timu kupoteza.
“Nimeiona mechi ilikuwa nzuri, lakini mbaya kwa sababu timu imepoteza. Ila niseme ukweli kama Simba ndio hii basi si timu ngumu kabisa. Wanacheza kawaida sana na hata kushinda kwao ni mapungufu yetu ya kiufundi,” alisema Zahera.