Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea kesho kwa mechi mbili, Mtibwa Sugar wakiwakaribisha Yanga SC Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro na Mbeya City wakimenyana na Tanzania Prisons katika mechi ya mahasimu wa Jiji la Mbeya.
Yanga SC itarejea Dar es Salaam kesho baada ya mchezo huo, kwa ajili ya mechi ya Kundi D Kombe la Shirikisho dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda.
Yanga ilianza vibaya michuano ya Kombe la Shirikisho kwa kufungwa mabao 4-0 na wenyeji, U.S.M. Alger katika mchezo wake wa kwanza wa Kundi D Kombe Jumapili Uwanja wa Julai 5, 1962.
Baada ya mechi Rayon Sport katikati ya wiki ijayo, michuano ya Kombe la Shirikisho itasimama kupisha Fainali za kombe la Dunia mwezi ujao nchini Urusi. Yanga watakamilisha mechi zao za mzunguko wa kwanza kwa kuwafuata Gor Mahia mjini Nairobi Julai 18.
Mzunguko wa pili Yanga itaanzia nyumbani Julai 29 na Gor Mahia, kabla ya kuwakaribisha na USMA Alger Agosti 19 na kwenda kumalizia ugenini Agosti 29 na Rayon.
Hiyo ni baada ya jana Simba SC kuendeleza wimbi la ushindi kwa kuwachapa wenyeji, Singida United 1-0 katika mchezo wa ligi hiyo uliofanyika Uwanja wa Namfua jioni ya leo.
Pongezi kwake mfungaji wa bao hilo la leo, beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Shomari Salum Kapombe dakika ya 23 aliyefumua shuti baada ya kukutana na mpira uliookolewa na kipa wa Singida, Ally Mustafa ‘Barthez’ kufuatia shuti la Nahodha, mshambuliaji John Bocco.
Ushindi huo unaifanya Simba SC ifikishe pointi 68 baada ya kucheza mechi 28 na kuzidi kuunenepesha ubingwa wake, iliyoutwaa rasmi Alhamisi baada ya mahasimu wao, Yanga kufungwa 2-0 na Tanzania Prisons mjini Mbeya.
Simba SC itateremka tena dimbani Mei 20 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kumenyana na Kagera Sugar katika mchezo ambao ndiyo watakabidhiwa taji lao la ubingwa wa Ligi Kuu kabla ya kwenda kuhitimisha msimu wa 2017-2018 kwa kumenyana na Maji Maji mjini Songea Mei 28.
Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, Kagera Sugar wameichapa Njombe Mji FC mabao 3-1 Uwanja wa Kaitaba Bukoba. Mabao ya Kagera yamefungwa na Jaffar Kibaya, Edward Christopher na Japhet Makalai, wakati la Njombe limefungwa na Notikel Masasi.
Ushindi huo unaifanya Kagera Sugar ifikishe pointi 31 katika mechi ya 28 na kupanda kwa nafasi tatu hadi ya 10 wakati Njombe Mji FC inaendelea kuzibeba timu nyingine 15 zilizopo kwenye Ligi Kuu kwa pointi zake 22 za mechi 28 pia.