SAINI ya winga Shiza Kichuya imewaingiza vitani matajiri wawili wakubwa nchini, Said Salim Bakhresa anayeimiliki Azam FC pamoja na bilionea wa Simba, Mohammed Dewji (Mo Dewji).
Iko hivi! Kichuya anamaliza mkataba wake ndani ya klabu hiyo msimu huu na wenyewe wanataka kumuongezea mkataba mpya, lakini wakati wakifikiria kufanya hivyo, Azam FC wanapanga kuingia mlango wa nyuma na kumnyakua.
Taarifa za ndani kutoka Azam FC, zinadai kuwa wamefanya mazungumzo na Kocha Mkuu wa Singida United, Hans van der Pluijm, ili kumchukua na yeye amekubaliana naye huku akiwaambia chaguo lake la kwanza ni Kichuya.
“Mazungumzo na Pluijm yanakwenda vizuri na yeye amesema anataka kuijenga upya Azam FC, huku akimtaja Kichuya (Shiza) kama chaguo lake la kwanza,” alisema kigogo mmoja ndani ya Azam.
DIMBA lilimtafuta meneja wa mchezaji huyo, Madundo Mtambo, ili kujua nini kinaendelea, naye alisema mpaka sasa si Simba wala Azam FC waliokaa meza moja na mteja wake huyo japo ana uhakika siku chache zijazo mambo yatakaa sawa.
“Kipindi hiki cha usajili mambo mengi yanazungumzwa ila yote kwa yote niseme tu hatujakaa na timu yoyote, japo natarajia kuwa siku si nyingi kila kitu kitakuwa wazi,” alisema.
Kama kweli Azam wanamuhitaji Kichuya, hiyo itakuwa vita ya matajiri hao wawili, Bakhresa ambaye atataka kuonyesha jeuri yake ya fedha pamoja na Mo Dewji ambaye hatataka winga huyo aondoke kienyeji.