Rais John Magufuli amewataka wanafunzi wa vyuo vyote nchini kuzingatia masomo badala ya kujihusisha na masuala ambayo ni kinyume na masomo yao ikiwemo siasa na kufuata mkumbo.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo May 07, 2018 akiwa ziarani mkoani Morogoro katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), ambapo amesisitiza watakaoshindwa kufanya hivyo watachukuliwa hatua zinazostahili.
“Bahati nzuri mnaenda vizuri, msivigeuze vyuo vikawa maeneo ya kufanya siasa. Maeneo ya vyuo ni kusoma na kufanya utafiti, hilo ndilo ombi langu,” amesema.
“Nataka niwaeleze kiukweli kama patatokea chuo chochote kitafanya fujo, mimi huyo wala sitasita kufukuza na nikifukuza sifahamu nitarudisha lini ili kusudi makajifunze namna ya kusoma, hili siwatishi nawaeleza ukweli,” amesisitiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli ameeleza kuwa serikali imetoa mikopo kwa wanafunzi 6, 600 fedha ambazo zimekusanywa kutoka kwa watu masikini hivyo atasikitishwa na wanafunzi ambao watafanya mambo kinyume na ya yaliyowapeleka chuo.