Ibrahim Ajib, Papi Tshishimbi, Thabani Kamusoko na Amissi Tambwe ni miongoni mwa wachezaji ambao bado wana mikataba iliyo hai na klabu ya Yanga.
Kuna tetesi kwamba Simba inajaribu kumsajili Mcongo Papi Tshishimbi lakini ukweli ni kwamba Tshishimbi hasajiliki bila ya Yanga kutoa ruhusa kwa kuwa bado ana mkataba ulio hai.
Ili kuweza kumpata, Simba watalazimika kuwasilisha ofa yao kwa uongozi wa Yanga ambao kimsingi ndio wenye maamuzi juu ya mchezaji huyo.
Ninachofahamu Simba na Yanga hazijawahi kuwa na utamaduni wa kuuziana wachezaji ambao mikataba yao haijamalizika.
Wachezaji wote wanaotoka upande mmoja kwenda mwingine mikataba yao inakuwa imemalizika.
Yanga ilitumia mfumo huo kuwapata Kessy na Ajib msimu uliopita wakati Tambwe alisajiliwa baada ya kukatwa kwenye usajili wa Simba dakika za majeruhi.
Ni hivyo hivyo Simba iliweza kumsajili Haruna Niyonzima kutoka Yanga msimu uliopita
Hata Donald Ngoma ameondoka Yanga na kutua Azam FC baada ya pande zote mbili kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba wake wa miaka miwili, hakuuuzwa.
Yanga ina wachezaji 10 waliomaliza mikataba yao ambao ni Kelvin Yondani, Hassani Kessy, Juma Abdul, Andrew Vicent na Obrey Chirwa.
Wengine ni Nadir Haroub, Benno Kakolanya, Emanuel Martin, Said Juma Makapu na Geofrey Mwashiuya.
Uongozi wa Yanga umesema kocha Mwinyi Zahera ndiye mwenye uamuzi wa mwisho juu ya hatma ya baadhi ya wachezaji ambao mikataba yao imemalizika