Uongozi wa Yanga unatarajia kufanya kikao na wachezaji wake kabla ya kuikaribisha Rayon Sports kutoka Rwanda katika ya hatua ya makundi ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga itakuwa uwanja wa Taifa kesho Jumatano kuwakaribisha Rayon Sport katika mechi ya pili ya Kundi D itakayofanyika kuanzia saa 1:00 usiku.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano wa Yanga, Hussein Nyika, amesema hawataki kuona wanapoteza tena mchezo wa kesho ambayo unafanyika nyumbani, ndio maana wanajiandaa kupanga mikakati ya ushindi.
"Kikubwa tunataka kurudisha morali ya wachezaji wetu, tumevuliwa ubingwa wa Ligi Kuu, sasa tunaelekeza nguvu kwenye michuano ya kimataifa, tumepoteza mchezo wa kwanza ugenini dhidi ya USM Alger, hatutaki kupoteza tena mchezo hasa kwenye uwanja wa nyumbani."
Yanga itaikaribisha Rayon Sports ikiwa na kumbukumbu ya kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa USM Alger kwenye mchezo wa kwanza wa kundi D.