Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe amefungua Mkutano Mkuu wa Wanachama wa klabu ya Yanga uliofanyika leo kwenye ukumbi wa Bwalo la Polisi, Masaki jijini Dar es salaam.
Akizungumza kwenye Mkutano huo, Dk Mwakyembe amewataka wanachama wa klabu ya Yanga kutumia nafasi waliyoipata leo kuirejesha heshima ya klabu yao.
Dk Mwakyembe amesema yaliyoikumba Yanga wakati huu hayapendezi hasa ukizingatia heshima ya kipekee iliyonayo klabu hiyo.
"Yanga SC ni moja ya alama za Uhuru wa nchi hii. Ikifungwa au kuyumba inaumiza wengi. Naamini mkutano huu utafanya maamuzi sahihi kwa mustakabali chanya wa klabu na soka letu kwa ujumla," amesema Dk Mwakyembe.
"Kwa msiofahamu, Yanga imechaguliwa kuwa alama ya ukumbusho barani Afrika, kama moja ya vilabu vilivyobeba alama ya uhuru wa Tanzania na uhuru wa bara la Afrika.
"Yanga ni klabu kubwa na yenye historia yake ndani ya nchi hii, acheni kuichukulia mzaha mzaha tu inafungwa mpaka na vitimu vidogo"
"Ikifungwa Yanga tunaumia wengi, ndani na nje ya nchi. Yanga ndio alama ya uhuru wa nchi hii. Naamini mkutano wa leo utafanya maamuzi yaliyo sahihi kwa mstakabali mwema wa soka la Tanzania," amesema Dk Mwakyembe
Wakati huo huo Waziri Mwakyembe ameupa uongozi wa klabu ya Yanga siku 60 kuhakikisha umefanya uchaguzi kujaza nafasi zilizowazi.
Mkutano huo umeendelea bila ya waandishi wa habari baada ya Waziri kuondoka.
Katibu Mkuu wa Yanga Charles Mkwasa amesema kuna maswala yanapaswa kujadiliwa kisha kufanyiwa maamuzi na Wanachama pekee.
Taarifa ya maazimio ya Mkutano huo itatolewa baadae.