KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ameamua kukata mzizi wa fitina Jangwani, huku wanachama wa Yanga wakijiandaa kufanya Mkutano Mkuu wao, ili kujua kama bilionea Yusuf Manji anarejea kuwatoa kwenye dhiki ama la.
Yanga inafanya mkutano wake leo kwenye Bwalo la Polisi, Oysterbay jijini Dar es Salaam na mbali na yote yatakayojiri lakini kutua au kutotua kwa Manji mkutanoni ndio kutatoa picha kamili ya mafanikio ya Yanga.
Yanga wanakutana katika mkutano huo wa kwanza leo kwa mwaka huu na mbali na ajenda zote zilizopangwa, homa ya mkutano huo itakuwa ni kusubiri kuona kama Manji anawasili katika mkutano huo.
Wanachama wa Yanga wamepanga kufurika katika mkutano huo kwa wingi wakitaka kusikia kauli ya mwenyekiti wao huyo aliyejiweka kando mwaka mmoja uliopita na kuiachia klabu yao majanga. Haijafahamika rasmi kama Manji atafika au la, lakini Mwanaspoti linafahamu mabosi wa juu wa klabu hiyo hususan wale wa Baraza la Wadhamini walikuwa wakihaha kuhakikisha kigogo huyo anatua katika mkutano huo.
Kutua kwa Manji katika mkutano huo kutalainisha ajenda zote za mkutano huo na kuufanya umalizike kwa utulivu mkubwa na kiu ya wanachama wa klabu hiyo ni kuona bilionea huyo anatoa picha kamili kwao kama anarejea au vinginevyo.
Tayari Yanga imeshatangaza ajenda za mkutano huo lakini ajenda muhimu ni uelekeo wa kubadili mfumo wa uendeshaji wa klabu.
Mapema juzi zilienea tetesi mkutano huo ulikuwa hatarini kuzuiwa mahakamani habari iliyowashtua mabosi wa klabu hiyo, lakini mpaka jana walijihakikishia mipango hiyo ilikwama na mambo yataendelea kama kawaida kuianza saa 4 asubuhi.
Katika hatua nyingine Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ameamua kukata mzizi kwa kutamka, katika usajili wake ujao anataka kila nafasi inakuwa na nyota bora wawili au zaidi ili kuondoa wachezaji wasumbufu kikosini.
Akizungumza na Mwanaspoti Zahera alisema ameshtuka kuona kuna baadhi ya nyota wa kikosi hicho wakiwa wasumbufu kwa vile wamekosa washindani katika nafasi wanazocheza na kuifanya timu iyumbe.
“Unapokuwa na timu ambayo haina usawa ni rahisi kuona baadhi ya wachezaji wakipoteza weledi na kuanza kusumbufu mara leo aje mazoezini au asije, lakini kunapokuwa na ushindani mzuri wa namba hawataweza kufanya kitu cha namna hiyo,” alisema kocha huyo raia wa Congo.
Katika hatua nyingine straika Mbenini, Marcelin Degnon Koupko, ametua nchini juzi ili ajaribiwe Yanga, lakini akipishana na Zahera anayeenda Ufaransa kwa mapumziko mafupi. Koupko alipokewa na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Dismas Ten.