MWANAFUNZI wa Chuo cha St. Joseph, Tawi la Luguruni jijini Dar aliyejulikana kwa jina la James John Tumati (pichani) aliyekuwa anasomea kozi ya ualimu katika ngazi ya stashahada, ameuawa kinyama na watu wasiojulikana kwa kuchomwa kisu alipokuwa anatoka kula saa tano usiku katika eneo la Makondeko nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Mei 31 mwaka huu, Mtaa wa Lopasi ambapo marehemu akiwa na wenzake wawili baada ya kula akawa katika matembezi maeneo ya Makondeko saa 5 usiku wakavamiwa wakavamizi na watu wawili waotaka wapewe pesa.
Akizungumza huku akitokwa machozi na Gazeti la Uwazi, shuhuda wa tukio hilo na rafiki wa James, Stanford Mshana alisema kuwa walikutana na watu hao wawili waliotaka wawape pesa kwa nguvu na walijaribu kupambana nao lakini walishindwa kufuatiwa kuzidiwa nguvu.
“Tulikuwa tunatoka kula ilikuwa kama saa tano usiku, nilikuwa mimi pamoja na rafiki yetu mwingine, jumla tulikuwa watatu na tulipovamiwa palikuwa siyo mbali na tunapoishi, ila eneo lenyewe halikuwa na mwanga.
“Tukakutana na hao watu wawili wakatuambia kwamba tuwape pesa, sisi tukawaambia hatuna, wakaanza kututisha, mmoja akatoa kisu ndipo mimi nikakimbia lakini mwenzangu James aliendelea kupambana nao.
“Sisi tulikimbia baadaye tulirudi kumuangalia mwenzetu tukakuta anavuja damu eneo la kifua na ameishiwa nguvu, tukamuwaisha Hospitali ya Boch na daktari alipompima wakagundua kuwa mechomwa kisu na akatuambia tayari ameshafariki dunia,’’ alisema Stanford huku akilengwalengwa na machozi.
Mlezi wa wanafunzi katika chuo hicho, Isaya Mwaipopo alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na akasema mwanafunzi huyo alikuwa anasoma kozi ya ualimu.
“Tulipata taarifa kwamba James ambaye alikuwa na wenzake, maeneo ya Makondeko walipokuwa matembezini saa tano usiku walivamiwa na majambazi,sasa katika purukushani, marehemu alichomwa kisu kifuani kilichosababisha kifo chake,” alisema Mwaipopo.
Naye Waziri wa Habari na Mawasiliano wa Serikali ya Wanafunzi chuoni hapo, Raphael Nyatega, alisema amepokea taarifa za kifo cha James kwa masikitiko makubwa na anauomba uongozi wa chuo uliangalie kwa jicho la tatu suala hilo ili iwe changamoto na kuweza kujenga mabweni ya chuo kwani hakina mabweni na wanafunzi wamepanga maeneo ya jirani.
Shemeji wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Gabriel Ngowi alisema wamepokea kwa mshtuko mkubwa kifo hicho, hata hivyo, amewashukuru viongozi wa chuo na wanafunzi kwa kutoa mchango wa gari kwa ajili ya kwenda kwenye mazishi Babati mkoani Manyara yaliyofanyika Juni 2 mwaka huu.
“Hili ni pigo kubwa sana kwa familia kwa sababu james alikuwa mwaka wa mwisho ili aweze kujitegemea na ili aweze kuisaidia familia kwa kuwa yeye ni mtoto wa kwanza wa kiume kwa wazazi wake,” alisema Gabriel.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ACP Jumanne Muliro hakuweza kupatikana kwa njia ya simu kwani alipopigiwa mara kadhaa iliita tu.
Source:Global publisher