BREKING : MAMA, BINTI YAKE WAUAWA KINYAMA, WATUMBUKIZWA CHOONI
WAKATI tukio la Mwandishi na Mhariri wa Gazeti la Kingereza la The Guardian, Finnigan Simbeye kuokotwa akiwa hajitambui huko Bunju jijini Dar likiibua mambo mazito, mama mwenye umri wa miaka 70, Lightness Mavura na bintiye Judica Msuya (37) pichani, wanadaiwa kuuawa kinyama, Uwazi lina kisa na mkasa wa kutisha.
Simbeye aliokotwa juzi, Jumapili asubuhi akiwa hajitambui na majeraha yaliyoonesha kupigwa mno hivyo kuibua gumzo huku mama huyo na bintiye miili yao ikikutwa kwenye shimo la choo.
Bunti.
TUKIO LA MAMA NA BINTIYE
Kwa mujibu wa mashuhuda wetu, mama na bintiye huyo, wakazi wa Kijiji cha Msangeni, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro waliibua sintofahamu baada ya miili yao kukutwa kwenye shimo la choo ikiwa imeharibika na kutoa harufu kali iliyokuwa imesambaa.
Mashuhuda hao walilieleza Uwazi kuwa, miili hiyo iligundulika hivi karibuni baada ya ndugu kutowaona wawili hao kwa muda mrefu huku nyumba yao ikibaki mlango wazi.
MTOTO WA MAREHEMU ANENA
Mmoja wa watoto wa marehemu, Daimael Msuya aishiye jijini Arusha alilieleza Uwazi kwamba, alifika nyumbani kwa mama yake huyo, Machi 22, mwaka huu kwa lengo la kumjulia hali baada ya kutopatikana kwenye simu yake ya mkononi kila alipompigia hivyo akaona aende kujua kulikoni kwani haikuwa kawaida yake kutopokea simu.
“Nilipofika nyumbani kwa mama yangu, nilishangaa kukuta mlango ukiwa wazi na mazingira ya ndani yalikuwa machafu mno, kinyume na nilivyozoea kuikuta nyumba ikiwa safi,” alisema Daimael.
MBUZI WADHOOFU
Alisema kuwa, katika kuzunguka kutazama mazingira ya nyumbani hapo alipigwa na butwaa kukuta mbuzi wanaofugwa na mama na bintiye huyo wakiwa bado wamefungiwa ndani huku hali zao zikiwa zimedhoofu.
Alieleza kuwa, jambo hilo lilimtia shaka na kumlazimu kuomba msaada kwa majirani na ndugu zake wengine ili wafike nyumbani kwa mama yake akitaka kujua kilichokuwa kikiendelea nyumbani hapo na kwamba hakumkuta mama na dada yake hivyo alitaka kujua walipo.
Daimael alisema kuwa, mara baada ya ndugu na jirani kufika, walianza kumtafuta marehemu na mwanaye, walipozunguka nyuma ya nyumba, walisikia harufu isiyo ya kawaida na walipofuatilia waligundua kuwa ilikuwa ikitokea kwenye shimo la choo lililopo nyumbani hapo.
TOCHI ILIVYOTUMIKA
Alisema kuwa, baadaye waliamua kumulika na tochi ndani ya shimo hilo ndipo walipoiona miili ya marehemu hao ikiwa imeharibika vibaya na kuwa ndiyo iliyokuwa ikitoa harufu kali nyumbani hapo.
Daimael alieleza kuwa, baada ya kubaini miili hiyo walitoa taarifa polisi ambao walifika na kuitoa miili hiyo kisha kuifunga kwenye mifuko ya nailoni kutokana na kuharibika na kutoa harufu kali kisha kwenda kuihifadhi kwa ajili na uchunguzi na taratibu za mazishi.
NDUGU WAKAMATWA
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linawashikilia watu watatu ambao ni ndugu wa marehemu hao wanaoshukiwa kuhusika na tukio hilo.
KAMANDA WA POLISI
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, SACP Hamisi Issah aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni mkwe wa marehemu aitwaye Samweli au Mtumishi, Paulo Robert na Sadiki Robert ambao ni watoto wa kaka yake mama marehemu.
Hata hivyo, taarifa zaidi zilidai kwamba, kabla ya tukio hilo watuhumiwa hao walikuwa na mgogoro wa kifamilia na marehemu Lightness hivyo ndugu wa familia hiyo waliomba uchunguzi ufanyike na haki ipatikane kwani ni tukio la kinyama zaidi kutokea kijijini hapo.
TURUDI TUKIO LA MWANDISHI
Tukirudi kwenye tukio la Mwandishi na Mhariri wa Gazeti la The Guardian, Finnigan Simbeye, jamaa huyo aliokotwa juzi Jumapili asubuhi huko Bunju nje kidogo ya Jiji la Dar akiwa hajitambui na majeraha yaliyoonesha kupigwa mno.
Taarifa kutoka kwa mashuhuda zilieleza kuwa, Simbeye aliokotwa akiwa katika hali mbaya huku akiwa na majeraha ya kipigo, jambo lililozua mjadala mzito huku wengine wakidai huenda alitekwa na wasiojulikana kisha kumtesa na kwenda kumtupa maeneo hayo.
Wengine walikwenda mbali zaidi na kuhusisha mfuko wa kiroba cha sandarusi kilichokuwa eneo la tukio kuwa huenda ndicho kilitakiwa kutumika kumfunga na kwenda kumtupa baharini.
Kwa mujibu wa mkewe, Rosemary Mirondo, mumewe huyo aliondoka nyumbani siku ya Jumamosi asubuhi na hakurejea hadi alipopigiwa simu kuwa ameokotwa akiwa hajitambui na kwamba polisi waliokuwa doria kwenye eneo hilo ndiyo waliompeleka katika Hospitali ya Mwananyamala, Dar kwa ajili ya matibabu.
KAMANDA MULIRO
Akizungumza na Uwazi juu ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Jumanne Muliro alisema kuwa, uchunguzi ulibaini kuwa mtu huyo alikuwa amelewa hivyo kuwashangaa na kuwapuuza wanaolihusisha tukio hilo na mambo ya utekaji wa wasiojulikana.
Alisema kuwa, jeshi hilo linaendelea na uchunguzi na kama itabainika kuwa alikuwa amelewa kupita kiasi na kulala barabarani litamchukulia hatua za kisheria kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.