Douma: Uwanja wa ndege za kivita wa Syria washambuliwa kwa makombora

Watu kadha wamefariki katika uwanja mmoja wa ndege wa kijeshi nchini Syria baada ya shambulio la kutumia makombora, vyombo vya habari vya serikali ya Syria vinasema.
Shirika la serikali la SANA limesema makombora kadha yalirushwa uwanja wa ndege wa Tayfur, ambao pia hufahamika kama T4 karibu na mji wa Homs, mapema leo Jumatatu.
Maelezo zaidi bado yanaendelea kutolewa lakini bado kufikia sasa haijafahamika nani amehusika.
Shambulio hilo limetekelezwa huku jamii ya kimataifa ikiendelea kulaani shambulio la kemikali ambalo lilitekelezwa katika mji wa Douma ambao unashikiliwa na waasi.
Rais wa Marekani Donald Trump alimweleza Rais wa Syria kama "nduli" Jumapili na kuonya kwamba yeye pamoja na washirika wake Iran na Urusi "watalipia sana".