Familia ya Lowassa yazungumza kuhusu mwanamke aliyedai ni ndugu yao
Familia ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Lowassa imeibuka na kueleza kushangazwa na mwanamke aliyekwenda Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kudai kuwa ni mtoto wa kiongozi huyo.
Kauli ya familia imetolewa na Fred Lowassa ambaye ni mtoto mkubwa wa Mzee Lowassa na kueleza kwamba, wameshangazwa na kitendo kilichofanywa na mwanamke huyo.
Kufuatia wito uliotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akitaka wanawake wote waliotelekezwa kufika ofisini kwake, mwanamke huyo aliyejitambulisha kwa jina la Fatuma Lowassa alifika ofini hapo na kusema kwamba yeye ni mtoto wa Lowassa na amekuwa akimtafuta baba yake huyo tangu akiwa darasa la sita.
Aliendelea kueleza kuwa, kwa muda wote huo amekuwa akifuatilia bila mafanikio yoyote ndio sababu ameamua kwenda kwa RC Makonda akiamini kwamba atapata msaada na kwamba yupo tayari kupimwa vinasaba (DNA) ili kuthibitisha kuwa yeye ni mtoto wa Lowassa.
Fred alisema kwao wao mtoto ni baraka na kwamba anashangaa mwanamke huyo kwenda kujitambulisha na kuachafua ukoo mzima kwani kwa desturi zao, huwa hawakati watoto. Aidha, amekosoa utaratibu unaotumiwa na RC Makonda na kumtaka kukumbuka mbali walipotoka kisiasa.
“Nimesikia mwanamama mmoja akiongea kuwa yeye ni ndugu yetu kule Dar es Salaam..Kwa taarifa tu sisi watu wa Monduli kwetu watoto ni baraka na neema, nimeshangaa ametukosa ukoo mzima kujitambulisha.. Namwambia Paul Makonda, nimetoka naye mbali sana, nasikitika sana anavyotumia nafasi yake vibaya kwa manufaa anayoyajua. Makonda nimekulea.”aliandika Fred.