SHULE ZILIZO TAIFISHWA HAZITAREJESWA- RAIS MAGUFULI
RAIS John Magufuli amesema shule, hospitali na vitega uchumi vingine vilivyokuwa vikimilikiwa na taasisi za dini nchini na kutaifi shwa wakati wa Azimio la Arusha mwaka 1967, havitarejeshwa kwenye taasisi hizo.
Rais Magufuli alisema hayo juzi wakati wa hafla ya kumsimika Askofu Mkuu mpya wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Isaac Amani iliyofanyika kwenye Parokia ya Mtakatifu Theresa mjini Arusha.
Rais alisema miradi iliyokuwa ikimilikiwa na taasisi hizo za dini, kama vile makanisa na misikiti, haitarejeshwa kwenye miliki za taasisi hizo. Alikiri kupokea maombi kadhaa ya viongozi wa dini, wakimuomba kurejeshewa vitega uchumi vyao hivyo.
Alisema, hata Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliwahi kumwandikia barua iliyoorodhesha mali za kanisa zilizotaifishwa wakati wa Azimio hilo la Arusha na kumwomba Rais azirejeshe mali hizo kanisani. Kardinali Pengo ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
“Hata Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alishaniomba nirejeshe mali za Kanisa la Katoliki kwenye miliki za kanisa, ila jibu ni hapana,” alisema Magufuli. Awali kabla ya hotuba ya Magufuli, Padre Kitomari wa Parokia hiyo alimwomba Rais kuirejesha mikononi mwa Parokia hiyo, Shule ya Msingi Naura, iliyopo eneo la Parokia, ambayo awali ilikuwa ikimilikiwa na kanisa hilo, lakini kwa sasa ipo chini ya serikali.
Katika maombi yake, alielezea sababu kadhaa za kuomba shule hiyo irejeshwe mikononi mwa kanisa na moja ya sababu hizo ni shule hiyo ipo kwenye eneo lenye hati ya Parokia, ambapo kwa sasa inaendelea na ujenzi wa majengo yake mapya.
Sababu nyingine ni kuwa matumizi mabaya ya uwanja wa shule hiyo, ambao unatumiwa na askari wa kikosi cha usalama barabarani (trafiki) mkoani Arusha, kama sehemu ya kuegeshea magari wanayoyakamata, kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani.
Kwa upande wa hoja hiyo, Magufuli alisema kuwa inaweza kuangaliwa kwa namna ya kipekee na kuwa akirejea Ikulu, ataifanyia kazi. Shule ya Naura ilijengwa mwaka 1950 na ilikuwa ikiitwa Shule ya Msingi ya Mtakatifu Theresia. Ilitaifishwa na serikali wakati wa Azimio la Arusha mwaka 1967.
Ilipobadilishwa iliitwa kwa jina la Naura, jina la mto unaopita karibu na shule hiyo. Kwa sasa shule hiyo ina wanafunzi 350. Lakini, Rais Magufuli alikataa ombi la Parokia hiyo la kutaka kupewa eneo la bustani ya Naura, kwa kuwa ni eneo la wazi. Kwamba Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 imesema kuwa maeneo yaliyo karibu na mito au maziwa, hayatakiwi kuguswa. Siyo viongozi wa Kanisa Katoliki tu, ambao wamekuwa wakiomba kurejeshewa shule zao, zilizotaifishwa na serikali, kwani hata Kanisa Anglikana nalo limekuwa na madai kama hayo.
Mwezi uliopita Kanisa Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, nalo lilimuomba Rais Magufuli kuwarejesheaa Shule ya Sekondari ya Minaki, iliyopo nje kidogo ya Dar es Salaam, katika wilaya jirani ya Kisarawe mkoani Pwani. Ombi hilo lilitolewa na Askofu mpya wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosthenes baada ya kusimikwa na kuwekwa wakfu katika Kanisa la Mtakatifu Albano, jijini humo.
Kwa mujibu wa askofu huyo, shule hiyo kongwe ya Minaki ni moja ya shule za Waanglikana, zilizotaifishwa na serikali. Askofu huyo wa Anglikana alitoa ombi hilo kwa Rais Magufuli, aliyehudhuria ibada kanisani hapo.