USHINDI DHIDI YA SINGIDA UNITED NI LAZIMA-WANAJANGWANI
Kesho Jumatano April 11 2018 Yanga itashuka kwenye uwanja wa Taifa kuikabiki Singida United kwenye moja ya michezo ya kuamua hatma ya ubingwa kwa Yanga.
Yanga inakumbana na Singida United kwa mara nyingine ikiwa ni baada ya siku tano kupita tangu wababe hao wa soka la Tanzania kuondoshwa katika hatua ya robo fainali ya kombe la FA na hao hao Singida United mkoani Singida.
Yanga itashuka uwanjani kulipa kisasi baada ya kipigo kile cha mikwaju ya penati.
Lakini pia Yanga inalazimika kushinda mchezo huo ili iendelee kuweka hai matumaini ya kutetea ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo.
Baada ya mchezo dhidi ya Singida United, Yanga haitakuwa na mchezo wowote wa ligi hadi baada ya kucheza na Wolaitta Dicha mchezo wa marudiano kombe la Shirikisho April 18.
Wakati Yanga ikitekeleza majukumu ya Kimataifa, Simba itacheza michezo miwili hadi mitatu zaidi kabla timu hizo hazijakutana kwenye mchezo baina yao April 29.
Ushindi dhidi ya Singida United utaifanya Yanga irejeshe tofauti ya pointi baina yake na Simba kuwa tatu baada ya Simba kuifunga jana Mtibwa Sugar 1-0 na kufikisha alama 52.