Uongozi wa Yanga tayari umekata rufaa kufuatia kilichotokea mkoani Mbeya jana kwenye mchezo wa ligi kuu ya Vodacom dhidi ya Mbeya City.
Mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 uligubikwa na vurugu kutoka kwa mashabiki wa Mbeya City hali iliyopelekea jeshi la Polisi kutumia mabomu ya machozi kuwasambaratisha mashabiki wa Mbeya City waliokuwa wakifanya vurugu jukwaani.
Mapema leo Katibu Mkuu wa Yanga Charles Mkwasa alisema tayari wamewasilisha rufaa yao TFF.
"Hakukuwa na sababu yoyote mchezo wa jana kuendelea baada ya dakika ya 69 kutokana na vurugu kubwa zilizojitokeza uwanjani, mashabiki wa Mbeya City wakirusha mawe na silaha nyingine."
“Wachezaji wangu walipatwa na wasiwasi na kupunguza kwa kiasi kikubwa fikra za kimchezo na zaidi wakicheza kwa hofu ya kuogopa kupigwa mawe, jambo ambalo liliwaruhusu wenyeji kuuteka mchezo hadi kupata bao la kusawazisha.”
“Kipa wetu, (Youthe Rostand) mara mbili aliliacha lango wazi na kwenda katikati kabisa ya Uwanja kunusuru maisha yake baada ya kuanza kushambuliwa kwa mawe na mashabiki wa Mbeya City, jambo ambalo refa na wasaidizi wake wote, hata Kamisaa waliona. Ni kwa sababu hizo tumekata rufaa,"amesema Mkwasa.
Lakini pia klabu ya Yanga imelalamikia tukio la Mbeya City kuchezesha wachezaji zaidi uwanjani.
Kamati ya Saa 72 inatarajiwa kukutana wiki hii, inatarajiwa rufaa hiyo ya Yanga itawasilishwa kwa Kamati hiyo.