HOUSE OF ENTERTAINMENT


JOIN KENYASWAHILINEWS
!-- AdsAgony - Ad Display Code -->

MPYA MPYA ZA LEO

HABARI (193) Michezo (121) BURUDANI (86)

Alhamisi, 3 Mei 2018

Jumapili imepita, Hassan Kessy anataka irejee upya


Ni mara ngapi ukikumbuka enzi za utoto wako au ujana wako, ungependa enzi hizo zirejee tena. Unakumbuka jinsi ulivyokuwa ukifurahia maisha na marafiki.

KUNA wakati huwa unapenda muda ujirudie katika maisha yako, lakini kwa bahati mbaya maisha hayarudi nyuma, yanakwenda mbele.

Ni mara ngapi ukikumbuka enzi za utoto wako au ujana wako, ungependa enzi hizo zirejee tena. Unakumbuka jinsi ulivyokuwa ukifurahia maisha na marafiki.

Lakini pia kuna enzi unapenda zirudi ili urekebishe mambo ambayo uliyakosea. Ungetamani kama dunia inaweza kurudi ili ujipange upya na usifanye kosa ambalo limeendelea kukutesa mpaka sasa.

Sisi kama binadamu, tumefanya makosa mengi na baadhi ya watu wameendelea kuteseka kwa makosa waliyoyafanya miaka 20 iliyopita.

Bila shaka hao nao wangependa dunia irudi kinyumenyume ikiwezekana warekebishe mambo yao ili wasiishi kama wanavyoishi sasa.

Kwa bahati mbaya sana hatuna hiyo nafasi na ndio maana unashauriwa kufanya mambo kwa kufikiria mara mbili huku ukiamini unachokifanya hakitakuwa na madhara.

Inawezekana kusiwe na Jumapili nyingine kama iliyokuwa juzi. Ndiyo inaweza isiwepo ya aina hiyo kwa watu wengi.

Mambo matatu yalikuwa yakiendelea siku hiyo; sherehe ya mwanamuziki wa kizazi kipya Ali Kiba ilikuwa inaonyeshwa na televisheni ya Azam, watani wa jadi Simba na Yanga walikuwa wakipambana kwenye Uwanja wa Taifa huku Manchester United na Arsenal wakikutana Old Trafford.

Ilikuwa siku ambayo kuna wengine wangependa irudi ili warekebishe mambo yao, lakini kuna wengine wasingependa siku hiyo irejee tena.

Kama ni shabiki wa Ali Kiba, Simba na Manchester United bila shaka utakuwa umeifurahia siku hiyo kwa sababu kulikuwa na ushindi sehemu zote.

Kwa mashabiki wa Ali Kiba ilikuwa ni siku kubwa, kwa mashabiki wa Simba ilikuwa ni zaidi ya ushindi, sasa wanaangalia ubingwa na kwa upande wa mashabiki wa Manchester United ilikuwa ni shangwe kwa sababu si kuifunga tu Arsenal, lakini walishuhudia kocha wao wa zamani Alex Ferguson akimuaga rasmi Arsene Wenger.

Ni Jumapili ambayo ilikuwa nzuri kwa wachache na mbaya kwa wachache pia. Lakini ilikuwa mbaya zaidi kwa Hassan Ramadhan Kessy.

Miaka miwili iliyopita, Kessy alitaka kupigwa na kipa wa Simba, Vicent Agban kwa sababu alikuwa amepewa kadi nyekundu katika mchezo muhimu dhidi ya Toto Africa.

Hakuna kiongozi wa Simba aliyekuwa anataka kusikia lolote kuhusu Kessy wakati huo, walikuwa wanataka aondoke, walimtuhumu kwa mambo mengi, kubwa ikiwa ni kuwa anatumika na Yanga.

Katika mechi fulani dhidi ya Yanga, Kessy alifanya kosa la mwaka ambalo lilisababisha Simba kufungwa.

Mashabiki na viongozi wa Simba hawajawahi kumsamehe.

Nilidhani amejirekebisha, kumbe Kessy ni yuleyule, inawezekana Simba walimtuhumu kwa kumuonea, lakini alibaki kuwa yuleyule.

Katika mechi ya juzi, Yanga waliingia uwanjani wakiwa dhaifu tofauti na Simba ambao wana kikosi kizuri msimu huu.

Yanga walihitaji nidhamu ya hali ya juu ili kupata angalau sare tu na Simba, lakini unapokuwa na mchezaji asiyejitambua kama Kessy unaweza vipi kulazimisha hata sare mbele ya kikosi bora cha Msimbazi.

Alichofanya Kessy ilikuwa ni kutojitambua, kwa sababu kadi zote mbili za njano hazikuwa na madhara yoyote hata kama asingefanya faulo.

Ni faulo ambazo alijitafutia na kuwapa wakati mgumu wenzake.

Ni Jumapili ambayo Kessy ataikumbuka zaidi kuliko mashabiki wengine wa soka, atapenda siku hiyo irejee ili airekebishe, lakini kwa bahati mbaya sana, dunia inakwenda mbele na hairudi nyuma tena.

Kwa uzembe ule wa juzi, nadhani Simba walimuonea Kessy kudhani anatumiwa na Yanga, kumbe ndivyo alivyo.

Kessy anatamani Jumapili irejee upya, ili arekebishe makosa yake, lakini hilo halitawezekana, kwa sababu saa zinasonga mbele huwa hazirudi nyuma.