Dar es Salaam. Kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, amegeuka dili kwa klabu za Yanga na Rayon Sports ya Rwanda, katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Wakati Yanga ilicharazwa mabao 4-0 na USM Alger, Rayon ililazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.
Timu hizo ziliteremka kwenye viwanja viwili tofauti juzi usiku na Mei 16 zitacheza mechi za raundi ya pili huku Yanga ikianzia nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Djuma alikuwa kocha wa Rayon na alitengeneza kikosi imara kabla ya kutua Simba akiwa msaidizi wa aliyekuwa kocha mkuu Mcameroon Joseph Omog.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Djuma alisema amezipa mbinu za ushindi timu zote mbili wakati zikijiandaa na mchezo wa raundi ya pili Mei 16.
Djuma jana aliipa Yanga siri za Rayon baada ya kufanya mazungumzo na gazeti hili kuhusu mbinu za kiufundi ambazo timu hiyo inaweza kutumia kupata ushindi katika mchezo huo.
Pia Masoud alidai kupigiwa simu na maofisa wa klabu hiyo kongwe nchini Rwanda wakitaka kujua mbinu za kiufundi za wawakilishi hao wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa.
Kocha huyo alisema Yanga na Rayon ni timu nzuri kwa kuwa kila moja inaundwa na wachezaji wenye viwango bora.
Djuma aliyeiongoza Royon kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Rwanda msimu uliopita, alisema Yanga inatakiwa kufanya maandalizi ya kutosha ili kupata ushindi.
“Yanga isiwe na wasiwasi baada ya kupoteza dhidi ya USM Alger, bado ina nafasi ya kufanya vizuri katika mashindano endapo itajipanga katika mechi na Rayon au Gor Mahia,” alisema Djuma.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Rwanda ‘Amavubi’, alidokeza kuwa Rayon imefanya usajili mzuri msimu huu ingawa hakuona mchezo wa juzi dhidi ya Gor Mahia.
Djuma alimtaja mchezaji tishio wa Rayon ambaye Yanga inakiwa kumpa ulinzi mkali Shasir Nahimana katika mchezo huo.
“Nimeifundisha Rayon kwa mafanikio, lakini sikubahatika kuona mechi yao na Gor Mahia kwa kuwa nilikuwa na majukumu ya timu yangu. Rayon imefanya usajili mzuri kama Simba, lakini timu yoyote inaweza kufunga au kufungwa,” alisema Djuma.
Kocha huyo alisema alipokuwa akifundisha Rayon alikuwa akimtua mshambuliaji mmoja au wawili kulingana na aina ya timu pinzani inayocheza dhidi yao.
Rayon inatumia mfumo 3-5-2 ambao Djuma aliutambulisha Simba baada ya Omog kuondoka.
“Siwezi kuzungumza kwa kina kuhusu mchezo wao kwa sababu Rayon ni timu ya nyumbani, siku yoyote nikiondoka Simba naweza kurejea kuifundisha, lakini kwa kifupi timu zote ni nzuri na zina nafasi ya kushinda,” aliongeza Djuma.
Kocha Mwinyi Zahera alisema Yanag ina nafasi ya kuzifunga Rayon na Gor Mahia, lakini wanatakiwa kurekebisha kasoro zilizojitokeza dhidi ya USM Alger.
“Kuna makosa tumefanya sipendi kuzungumzia tunatakiwa kurekebisha katika siku hizi zilizobaki kabla ya mechi ijayo. Unapocheza mechi moja ni mwanzo wa maandalizi ya nyingine jambo ambalo tunatazama.
“Nadhani kikubwa ambacho kitatusaidia katika mechi zijazo ni kufanya maandalizi ya uhakika, mazuri ya kiufundi ambayo yatatufanya tuwe imara na bora ili tupate ushindi,” alisema Zahera.
Kocha huyo alisema hajakata tama kwa kuwa amebakiza mechi tano zinazoweza kuipa nafasi ya kufuzu hatua ya robo fainali.
Baada ya kuvaana na Rayon, Yanga itakuwa ugenini kuikabili Gor Mahia Julai 18 kabla ya kurudiana na Gor Mahia Julai 29.
Ratiba Yanga itaikaribisha USM Alger Uwanja wa Taifa Agosti 19 kabla ya kwenda Rwanda kupepetana na Rayon Agosti 29.
M