Dar es Salaam. Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Shahada ya Famasia katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), amekutwa amekufa chumbani.
Taarifa kutoka chuoni hapo zinasema mwili wa mwanafunzi huyo, Edward Kahitwa ulikutwa chumbani jana Mei 19, 2018.
Imeelezwa Kahitwa hakuonekana hadharani tangu Alhamisi Mei 17, 2018 hadi mwili wake ulipogundulika kuwapo chumbani jana.
Alipotafutwa na mwandishi wa habari wa The Citizen, Ofisa Uhusiano wa Muhas, Hellen Mtui alithibitisha kifo cha Kahitwa na kueleza kuwa chanzo cha kifo chake bado hakijajulikana.
Tayari Kaimu mshauri wa wanafunzi Muhas, Dk Joseph Sempombe ametangaza kifo cha Kahitwa leo Mei 20, 2018, akisema chuo kitaendelea kutoa taarifa kuhusu tukio hilo.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa mwili wa mwanafunzi huyo ulikutwa ndani ya chumba chake namba 65 katika hosteli ya Kagera.
Imeelezwa polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo na mwili wa Kahitwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).