KAMA Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lisipochangamka, basi vipaji vitaendelea kunufaisha mataifa mengine hasa ya Ulaya.
Kinda la Kitanzania, Eddo Nyamsangya (17) anayekipiga SC Heerenveen na Ali Bwando (21) wa Roda JC Kerkrade wasipofuatiliwa mapema basi timu ya Taifa (Taifa Stars) itaendelea kuwategemea Mbwana Samatta na Simon Msuva pekee pale mbele kwenye eneo la ushambuliaji.
Eddo na Ali ni makinda ya Kitanzania wanaokuja kwa kasi katika vikosi B vya timu hizo mbili za Ligi Kuu Uholanzi, ambapo PSV Eindhoven yenyewe imetawazwa kuwa mabingwa wapya kwa mara ya 24 msimu huu.
Ali, ambaye jana Mei 6 alitimiza miaka 17, alisema kabla ya mchezo huo, anaweza kupewa nafasi ya kucheza kwenye mechi ya mwisho ya Eredivisie dhidi ya Feyenoord.
“Ndoto yangu ni kucheza mpira kwa mafanikio, karibu msimu mzima nimecheza ligi ya wachezaji wa akiba, sijui kama nitapandishwa au nitaendelea na kikosi B,” alisema Ali.
Ugumu wa Eddo kucheza mchezo wa jana ni mazingira ya timu yake ambayo ipo kwenye hatari ya kushuka daraja hivyo, huenda asipate nafasi kwenye kikosi cha kwanza kucheza mchezo huo.
Roda ilikuwa na kibarua kigumu jana dhidi ya ADO Den Haag na mara baada ya mchezo huo watacheza mchujo wa kupigania nafasi ya kusalia ligi kuu.
Ufafanuzi inshu ya Uraia
Uwezekano wa wachezaji wenye asili ya Kitanzania kuichezea Taifa Stars upo hata kama wamecheza kwenye mataifa mengine ngazi ya vijana.
Kanuni za soka zinaruhusu hilo, mfano mzuri ni sakata la winga wa zamani wa Manchester United, Wilfred Zaha ambaye aliichezea England kuanzia ngazi ya chini ya maika 19 hadi 21, lakini kutokana na ushawishi wa Ivory Coast aliamua kulitumikia taifa hilo.
Zaha ni mzaliwa wa Abidjan, Ivory Coast lakini tangu akiwa na miaka minne ameishi England na akachukua uraia wa nchi hiyo kanuni zilimruhusu kabla ya kuamua kuchana nao na kugeukia uraia wake wa zamani wa Ivory Coast.
Sources: mwanasport