HOUSE OF ENTERTAINMENT


JOIN KENYASWAHILINEWS
!-- AdsAgony - Ad Display Code -->

MPYA MPYA ZA LEO

HABARI (193) Michezo (121) BURUDANI (86)

Jumamosi, 19 Mei 2018

Matukio makubwa matatu ya mpira ambayo Rais Magufuli atashiriki leo


Rais Dkt John Pombe Magufuli leo anaweka historia kwa kushiriki katika matukio makubwa matatu ambayo yote yanahusu mpira wa miguu nchini.

Katika tukio la kwanza, Rais anatarajiwa kupokea Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, (CECAFA Challenge) kutoka kwa Timu ya ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys  waliloshinda mwaka huu nchini Burundi.

Serengeti Boys walitwaa kombe hilo baada ya kupata ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya Somalia katika mchezo wa fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Ngozi.

Ushindi huo ulitokana na mabao ya Edson Jeremiah dakika ya 25 na Jaffar Mtoo dakika ta 66 katika mchezo ambao Serengeti Boys ilionyesha kiwango cha hali ya juu na kuwafurahisha mashabiki.

Katika tukio la pili, Rais ataipokea Timu ya watoto wa kike wanaoishi katika mazingira magumu kutoka nchini Tanzania (TSC) iliyoshika nafasi ya pili kwa ubingwa dunia katika michuano hiyo iliyoandaliwa na Shirika la Street Child United na kufanyika nchini Urusi mwaka huu. 

Timu hiyo imeshika nafasi ya pili baada ya kufungwa goli 1-0 na timu ya Brazil katika fainali ya Kombe la Dunia (Street Children World Cup). Itakumbukwa kuwa mwaka 2014 nchini Brazil, timu ya wavulana walio kwenye mazingira magumu ilichukua ubingwa kwa kuifunga Burundi.

Tukio la mwisho ambalo pengine linasubiriwa kwa hamu zaidi kwa sababu ndio mara ya kwanza kufanyika, ni la Rais Dkt Magufuli kuikabidhi Klabu ya Simba, kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa mwaka 2017/18.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Mario Ndimbo, Rais Magufuli atawasili Uwanja wa Taifa Saa 8:00 na kukagua timu kabla ya mchezo kuanza Saa 8:15 na baada ya hapo atakabidhi Kombe kwa mabingwa, Simba.

Simba imetwaa kombe hilo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012.

Shauku ya wengi ni kutaka kuona kama Simba itaendeleza rekodi yake ya kutopoteza mechi kwa msimu huu ikimenyana na Kagera Sugar katika mchezo wake wa 29. Hadi sasa Simba imecheza michezo 28 ambapo imeshinda mechi 20 na kutoa sare 8.

Simba walitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Mei 10 baada ya mahasimu wao wa jadi, Yanga SC kufungwa 2-0 na Tanzania Prisons mjini Mbeya.