Tume ya Uchaguzi nchini Burundi imesema itatangaza matokeo ya kura ya maoni baadaye hii leo . Hata hivyo, Kiongozi wa upinzani nchini humo Agaton Rwasa amesema hatokubali matokeo ambayo yatatagazwa akitaja kuwa kura hiyo iligubikwa na udanganyifu mkubwa na vitisho kwa wafuasi wake.
Bwana Rwasa ameitaka tume ya uchaguzi kufutilia mbali matokeo na kuitisha kura mpya. Matokeo ya mwanzo yanaonyesha kuwa kura ya ' Ndiyo ' ya kuidhinisha marekebisho ya katiba imeshinda kwa kishindo.
Katiba hiyo ikiwa itaidhinishwa, itamuruhusu Rais Pierre Nkurunziza kuwania tena uongozi na kusalia madarakani hadi mwaka wa 2034.
Kulingana na risala iliyowasilishwa kwenye tume ya Uchaguzi, Agaton Rwasa na kambi yake ya Muungano wa Amizero y'Abarundi au Matumaini ya Warundi wanasema kura ya maoni haikuwa huru wala ya wazi. Akizungumza na BBC kwa njia ya simu.Kiongozi huyo wa upinzani anasema wafuasi wake walifanyiwa vitisho na vitimbi kuanzia kampeni hadi siku ya uchaguzi . Agaton Rwasa amesema hayuko tayari kukubali matokeo ya kura ya maoni yatakayotangazwa baadae hii leo.
Kwenye mazungumzo na gazeti la Ikiriho la karibu na utawala ,Makamu wa kwanza wa Rais Gaston Simdimwo ameyataja madai hayo kwamba ni uongo mtupu. Bwana Sindimwo amesema Itakuwa busara kama Rwasa na Kambi yake watakusanya na kuwasilisha ushihidi kwenye vyombo vya sheria vinavyoshughulikia malalamiko ya uchaguzi.
Kabla hata ya Agaton Rwasa kutishia kwamba hatakubali matokeo ya kura ya maoni kuhusu katiba, msemaji wa Tume ya Uchaguzi Prosper Ntaharwamiye alitupilia mbali madai ya wapinzani kuhusu dosari za uchaguzi huo.
''Ni makosa madogo madogo ambayo yalisahihishwa . Na ni matukio ambayo hayawezi kudosarisha uchaguzi. Hakuna wakala wa chama aliyefukuzwa kituoni. Mawakala wa vyama walisahihisha ripoti za matokeo ya kura. Kwa hiyo nasema kulikuwa na hitilafu ndogo ndogo , lakini shughuli ya kura ilifanyika vizuri''. Ntaharwamiye
Kwenye risala hiyo, Agaton Rwasa amesema ameanza kukusanya ushahidi tosha wa dosari kadha wa kadha kwenye uchaguzi huo wa kura ya maoni. Hayo yamejiri wakati tume ya Uchaguzi ikisema itatangaza matokeo hii leo alasiri.
Vyombo vya habari vya umma vimeshatangaza ushindi mkubwa wa kura ya Ndiyo ya kuidhinisha katiba wakitaja ushindi wa karibu ya asilimia 75 , matokeo ambayo yanapingwa vikali na upinzani.